KAMPUNI ya Tumbaku ya Alliance One Tanzania (AOTTL) iliyopo Morogoro imemkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Albert Msando, Mradi wa kisima na Madawati 300 vyote vikiwa na thamani ya Milioni 79 kwa ajili ya Shule ya Msingi Kingolwira iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Tukio hilo la hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa hivyo limefanyika leo Mei 27/2022 katika Shule ya Msingi Kingolwira na kushuhudiwa na Viongozi mbalimbali kutoka Manispaa ya Morogoro pamoja na Viongozi wa Kata na Wazazi wa wanafunzi.
Msaada huo umekabidhiwa Mkurugenzi wa fedha , Festo Mwalonga, akimwakilisha Mkurugenzi wa Alliance One kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro , Mhe. Albert Msando, katika halfa iliyofanyika Shuleni hapo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, DC Msando, amesema kwa upande wa mradi wa kisima utasaidia kutatua kero za maji shuleni pamoja na msaada wa madawati ambao utasaidia wanafunzi kukaa katika mazingira rafiki darasani.
DC Msando, amewapongeza Alliance One kwa kuwa karibu na Jamii jambo ambalo linapaswa kuigwa na Taasisi nyingine katika kurudisha gawio kwa jamii kama sheria inavyosema.
"Leo ndugu zetu wametukimbilia kutusaidia , na nimepata taarifa sio mara yao ya kwanza , niwaombe sana walimu endeleeni na moyo wa kufundisha kwani Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki lakini kwa Wazazi wote hakikisheni mnafunga mkanda kwa kushirikiana na waalimu ili kuhakikisha wanafunzi na watoto wenu wanafikia malengo waliojiwekea , suala la malezi msiwaachie waalimu lazima mshirikiane kikamilifu kama mnataka matokeo chanya" Amesema DC Msando.
Mwisho, DC Msando, ameutaka Uongozi wa Shule hiyo kuhakikisha wanatunza vizuri misaada wanayopewa na wafadhili na kuiwekea miundombinu mizuri ili iweze kuwasaidia katika kizazi cha leo na kesho.
Naye Mkurugenzi wa fedha Kampuni ya Alliance, Festo Mwalonga, ameipongeza Serikali kwa kuweka Mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji wa biashara nchini , hatua ambayo imefanikisha Kampuni yao ya Alliance One kuweza kuona inatoa misaada kwa jamii ikiwemo kusaidiana na Serikali.
Aidha, Mkurugenzi huyo wa fedha , amevitaja vitu vilivyotolewa ikiwamo Madawati 300 yenye thamani ya Shilingi Milioni 27,092,800.00 na Mradi wa Kisima wenye thamani ya Shilingi Milioni 52.
Ikumbukwe kuwa Alliance One sio mara ya kwanza kuisaidia shule hiyo kwani mwaka 2013 ilisaidia Shule hiyo Ujenzi wa Madarasa 2 na madawati 70 huku wakiendelea kuwa wadau muhimu katika kusaidia nyanja ya elimu.
Naye Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro , Chausiku Masegenya, amewataka waalimu kuweka mikakati ya pamoja ili kuongeza viwango vya ufaulu na ameishukuru Alliance One huku akiwataka kutokata tamaa ya kuendelea kuwasaidia kwani bado shule hiyo imekuwa na changamoto nyingi zinazoikabili.
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Kingolwira, Mh. Madaraka Bidyanguze, amesema Aliance One wamekuwa karibu nao kwa kila jambo na wamekuwa wepesi wa kusikiliza matatizo yao pale wanapokwenda kuomba msaada.
Mhe. Bidyanguze, ameomba wadau wengine kujitokeza kwa ajili ya kushirikiana na Serikali hususani katika kusaidia jamii ikiwamo huduma za elimu na masuala mengine mengine ya maendeleo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa