BENKI ya ABC Kanda ya Morogoro, imekabidhi vitu vyenye thamani ya zaidi ya milioni 2 katika kusaidia ujenzi wa Choo cha Walimu katika Shule ya Msingi Mtawala Manispaa ya Morogoro ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali kusaidia kuondoa changamoto zilizopo kwenye sekta ya elimu hususani katika upande wa vyoo.
Hafla hiyo fupi ya kukabidhi vifaa hivyo, imefanyika Aprili 20/2022 katika shule hiyo huku ikishuhudiwa na Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Morogoro , Chausiku Masegenya ,akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa.
Akizungumza Masegenya mara baada ya kupokea vifaa hivyo, ameishukuru Benki ya ABC huku akieleza kuwa msaada huo utagusa maisha ya Waalimu wengi kwa miaka mingi ijayo.
“Wadau wetu muhimu na washirika kama Benki ya ABC ndio nguzo muhimu kwa mafanikio yetu. Tunashukuru kwa msaada huu ambao utasaidia katika kuweka mazingira rafiki kwa waalimu ya kupata huduma ya choo , lakini pia kuwaondolea adha ya kutoka nje kwa ajili ya kufuata huduma ya choo" Amesema Masegenya.
Mwisho, Masegenya, ametoa wito kwa taasisi zingine za kifedha na wadau wanaopenda kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya vyoo pamoja na mazingira ya kujifunzia katika shule za umma zilizopo Manispaa ya Morogoro kujitokeza kwa wingi katika jitihada hizo.
Naye Diwani wa Viti Maalum kutoka Kata ya Mwembesongo, Mhe. Hadija Kibati, ameishukuru Benki ya ABC Kwa kuwaunga mkono kwenye sekta ya elimu kwa kuwapa vifaa hivyo ambayo yatasaidia kuondoa changamoto ya choo cha walimu shuleni hapo.
Kwa upande wa Meneja BANC ABC-Kanda ya Morogoro , Raphael Kalinga, akizungumza wakati wa halfa ya makabidhiano hayo, amesema kwamba utoaji wa misaada kwa jamii ni sehemu ya dhamira endelevu ya benki hiyo katika kusaidia sekta za elimu na kuona benki hiyo inachukulia kwa uzito sana suala la uwekezaji kwenye sekta ya elimu.
“Benki yetu inajivunia kuona Taifa linapiga hatua kubwa kwenye sekta ya elimu ambapo kupitia sera ya serikali elimu bure imeongeza idadi ya wanafunzi lakini pia ufaulu ambao maendeleo yake yanaakiisi hadi kiwango chetu cha uchumi ambapo mwaka jana nchi iliingia kwenye uchumi wa kati” Amesema Kalinga.
“Tumejitolea kuhudumia watu, biashara na jamii kwa ujumla. Benki yetu ya ABC, tumeguswa na changamoto ambayo iliwasilishwa kwetu , dhamira yetu kwa jamii ni kuona tunaunga mkono na kusaidia juhudi za kielimu na ustawi wa wanafunzi wetu na shule kote nchini na sio kwa Manispaa hii ya Morogoro pekee, hivyo ni muhimu zaidi tukiweka jitihada katika kuboresha mazingira ya vyoo shuleni ili sasa Waalimu waweze kuwa na mahala rafiki kwa kutumia na kuacha kutoka eneo lao kwenda mbali na shule zao, ABC tutaendelea kushirikiana na Serikali kwa kadri tunavyoweza kuguswa na changamoto katika jamii ” Ameongeza Kalinga.
Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mtawala, Mwl. Godfrey Binagwa , ameishukuru Benki ya ABC kwa msaada huo ambao wameutoa ambao utasaidia kuondoa changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo za uhaba wa choo cha walimu.
Vifaa hivyo vya ujenzi ambayo walikabidhi benki hiyo ni Mifuko 50 ya saruji, mchanga Lori 1, Kokoto Lori 1, Mawe Lori 1, Milango 2 ya mbao, Fremu 2 za milango, Tofali za block 400 pamoja na Mabati 70.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa