WAENDESHA Boda boda Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wameipongeza Manispaa ya Morogoro kupitia Idara ya Afya kwa jitihada za kuhamasisha na kutoa elimu juu ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti tofauti, wamesema tangia Serikali itangaze kuwepo kwa muathirika hapa nchini wamekuwa wakipewa elimu mara kwa mara jambo linalowafanya wazidi kuwa na amani na kuchukua tahadhari za mara kwa mara za kujikinga na Ugonjwa wa Corona.
Akizungumza kwa niaba ya Bodaboda wote, Katibu wa Bodaboda Mkoa wa Morogoro, Ndg. Juma Bega, amesema kitendo cha Manispaa kutenga muda wa kutembelea makundi maaalumu kama haya ya Vijana wao ni jambo jema na kuonyesha kwamba Serikali inawathamini Bodaboda na kuona kazi hiyo ni kama kazi nyengine zinazowaingizia vipato.
"Kwa kweli nichukue nafasi hii kwa niaba ya Uongozi wa Bodaboda Mkoa wa Morogoro, tunaipongeza sana Manispaa ya Morogoro hususani idara ya Afya chini ya ndugu yangu , Dr Ikaji Rashidi kwa kugawa maeneo ya kutolea elimu chini ya Wataalamu wake , hali hii imeonyesha upendo wa dhati na kuona sasa kundi hili linatambulika sana na kuweza kuokoa hata maisha ya Vijana wetu kwa kuwapatia Elimu hii ya kujikinga na Ugonjwa wa Corona, nampongeza sana Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mama yangu Regina Chonjo pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro dada yangu Sheilla Lukuba kwa kuchukua hatua madhubuti kabisa na kuunga mkono kauli ya Mhe. Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ya kutoa elimu na kuweka tahadahri kubwa katika nchi yetu ili kujikinga na Ugonjwa wa Corona" Amesema Bega.
Aidha , amewataka Bodaboda wote Mkoa wa Morogoro kuuchukilia Ugonjwa huo kwa umakini mkubwa na kuweka tahadhari za kujikinga wao na familia zao pamoja na abiria wanaowapakia kwa kunyunyiza dawa kwenye viti , mikono ya kushikia wakati wanaendesha pamoja na kupuliza dawa kwenye kofia zao na za abiria (elementi).
Kwa upande wa Mratibu wa Malaria na Magonjwa ya Watoto wenye umri chini ya miaka 5, Dr. Nicholaus Ntabaye akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, amesema kila Boda boda ni lazima ahakikishe chombo chake kabla ya kukitumia anakipulizia dawa ikiwamo viti, sehemu za kushikia mikono pamoja na kofia zao (elementi) ili kujikinga na Ugonjwa wa Corona.
"Nitoe wito kwa boda boda wote niwaombe msipuuzie haya maelekezo tumewafuata mlipo lengo letu ni kuwa karibu na wananchi wetu na kuangalia usalama wenu, zingatieni maelekezo ya wataalamu wanayowaambia huu ugonjwa sio mzuri hata kidogo wenzetu Mataifa ya nje wanateketea, tuwe makini sana na vyombo vyetu mara kwa mara tuviweke katika mazingira rafiki katika kujikinga na ugonjwa huu" Amesema Dr. Ntabaye.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa