MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema kero ya Dampo kwa sasa inakwenda kumalizika kufuatia kuweka kijiko kitakacho safisha njia na kuingiza takataka zote ndani ya Dampo hilo.
Akizungumza kuhusu kero hiyo, amesema kwa sasa kazi imeshaanza ya kuweka njia mbadala ambazo zitarahisisha magari ya taka kuingia katika dampo na kumwaga uchafu jambo ambalo awali lilikuwa changamoto kutokana na taka kutupwa nje ya dampo na kupelekea kero za kimazingira kwa wananchi.
"Ili kuondoa kero kwa wananchi ya harufu ya dampo na inzi wengi tumechukua uamuzi wa kukodisha kijiko kwa muda ili kuweka mazingira mazuri ya kuhakikisha takataka zote zinaingia ndani ya dampo, vifaa vyetu bado vinachangamoto lakini navyo tunavishughulikia vipo katika matengenezo, niwahakikishie Wananchi wa Manispaa ya Morogoro hakutazagaa takataka tena katika mitaa yetu na katika makazi ya wananchi , kwani magari yapo na dampo letu linaingilika kwa urahisi tofauti na awali " Amesema Sheilla.
Amesema kuwa, dampo hilo limekuwa likilalamikiwa nakusababisha uchafu kuingia mpaka barabarani na kusogea karibia na maeneo ya kazi za watu huku harufu mbaya ikiendelea kuwa kero kwa watu kila siku.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Manispaa ya Morogoro, Samweli Subi, amesema kuwa suala la uchafu katika Manispaa lipo ila
jitihada zinafanyika ili kupambana na suala la uchafu ambapo amewataka wale wanaohusika na ukusanyaji wa taka majumbani na mitaani wazidishe kasi kwani kwa sasa dampo hilo linapitika kirahisi tofauti na mwanzo.
Pia, amewataka wananchi kuhakikisha wanaweka mazingira safi na salama kwani Manispaa imejitahidi kununua mapipa ya kuhifadhia taka na kuyasambaza maeneo tofauti tofauti wakiwa na lengo la kuweka manispaa safi kwa ajili ya afya za wananchi wake.
Naye , Afisa afya na msimamizi wa dampo, Msisa Ziota, amemshukuru Mkurugenzi wa Manispaa kwa jitihada za kupata Kijiko mbadala cha kuchonga njia mbadala za kupitishia magari ya taka.
Amesema Kijiko hicho kipo kazini na tayari wameshaanza kuweka njia nzuri na magari ya taka yanaweza kuingia na kutupa taka katika dampo hilo kwa urahisi tofauti na awali
"Hatua nzuri sana, mwanzo hali ilikuwa mbaya takataka zote zilikuwa zinabakia nje nyingine zinaleta harufu katika makazi ya watu nzi wanazaliana wengi hususani katika kipindi cha mvua harufu inakuwa kali baada ya taka kuoza lakini kwa sasa magari yanapita kilichobakia ni kuweza kupata Wheel Loader ili kuchota taka zilizo pembeni mwa barabara na kuziingiza ndani baada ya hatua za awali ya kuzisogeza pembeni kuweka njia ya magari kupita"Amesema Ziota.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa