MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando, amepiga marufuku suala la uchepushaji wa maji katika vyanzo vya maji.
Kauli hiyo, ameitoa hivi karibuni, katika ziara yake ya kukagua vyanzo vya maji pamoja na mtambo unaosambaza maji uliopo eneo la Tumbaku Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, DC Msando, amesema kumekuwa na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji unaofanywa na wananchi kwa kuchepusha maji kutoka vyanzo vya maji.
Amesema kuwa wananchi wote ambao wamekuwa na tabia ya kuchepusha maji watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo faini pamoja na kifungo.
Aidha, DC Msando, amesema tayari katika Wilaya yake ameshaunda, kamati ya kufanya tathmini hiyo ili kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa na maji yanayopatikana yakawezeshe bwawa Mindu, kwa ajili ya kuzalisha maji na wananchi kupata maji kwa uhakika.
DC Msando, amewataka kila mwananchi kuhakikisha anakuwa msimamzi wa mazingira na anatunza vyanzo vya maji kwa kufuata sheria na taratibu ili kuhakikisha kila mtu anafikiwa na maji safi na salama kama haki ya msingi.
Naye, Mkurugenzi wa MORUWASA, Eng. Tamimu Katakweba, ametaka elimu kwa wananchi iendelee kutolewa hususani ya kutofanya shughuli za kiuchumi kando au pembezoni mwa mito na vyanzo vya maji ili kutoathiri upatikanaji wa maji.
Kwa upande wa Mhandisi wa rasilimali za Maji, Bonde la Maji Wami Ruvu ,akimwakilisha Mkurugenzi wa Bonde la Wami, John Kasambili, amewataka wananchi kila mmoja kwa nafasi yake kulinda miundombinu ya maji kwa kuwa wanaohujumu miundombinu hiyo wanafahamika kwakuwa wanaishi katika mazingira yao na pengine ni ndugu zao.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa