Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, mheshimiwa Rebecca Nsemwa akiwa ameambata na Kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, na baadhi ya wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa manispaa, MORUWASA, na TARURA, amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Mkundi, kwenye mtaa wa Mgulu wa Ndege kwa lengo la kusikiliza kero zao na kuzijibu.
Alipokuwa akizungumza kwenye mkutano huo tarehe 15.02.2024, mheshimiwa Nsemwa amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa macho mekundu (red eyes) kwa kuacha kushikana mikono, na kuhakikisha wananawa mikono mara kwa mara, kwa maji tiririka.
Pia, amewataka wananchi watambue kwamba ugonjwa wa kipindupindu umo ndani ya Manispaa hivyo waendelee kufuata maelekezo ya maafisa afya wanaopita kwenye mitaa yao na kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo.
Kwa upande wa wafanya biashara za vyakula, amewataka wafanye biashara hizo kwa kuzingatia utaratibu wanaoelekezwa na maafisa afya na kwamba ambaye hatafuata utaratibu basi biashara yake itafungwa.
Aidha, mhehsimiwa Nsemwa amewataka wazazi ambao watoto zao walifaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka huu, lakini mpaka sasa hawajawapeleka shule huenda kwa sababu wazazi wameshindwa kuwapatia mahitaji kama vile sare za shule,wahakikishe wanawapeleka shuleni watoto hao kwani Rais Samia anajitahidi sana kujenga shule na vyumba vya madarasa, na hakuna mtoto ambaye atafukuzwa shule kwa sababu ya kutokuwa na sare.
Mwisho, mheshimiwa Nsemwa amewataka wazazi kushirikiana na walimu katika malezi ya watoto wao ili kuwalinda na kuepuka matendo mabaya dhidi ya watoto kama vile ukatili wa kijinsia na unyanyasaji .
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa