Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia Wazee na Watoto,Mhe. Doroth Gwajima, amewataka Wazazi kuwapaeleka watoto wao katika vituo vya afya ili waweze kupatiwa chanjo.
Kauli hiyo ameitoa leo Aprili 27/2021 wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Chanjo Kitaifa ambayo imefanyika Mkoa wa Morogoro katika Manispaa ya Morogoro Kata ya Chamwino Viwanja vya Shule ya Msingi Chamwino B.
Aidha, Dkt.Gwajima, amesema kuwa watoto waliopata chanjo huwa wamekingwa dhidi ya magonjwa hatari, ambayo kwa kawaida huweza kusababisha ulemavu au kifo.
Amesema kuwa chanjo hutoa kinga dhidi ya magonjwa mengi hatarishi huku akisema kuwa Mtoto ambaye hajapata chanjo yuko katika hatari kubwa ya kupatwa na maradhi, ulemavu wa kudumu au hata kupoteza maisha.
“Watoto wote wana haki ya kupata kinga hii, ”Chanjo ni njia bora zaidi kuzuia magonjwa ya kuambukiza, hivyo Kila msichana na kila mvulana anapaswa kupata chanjo kamili. Kinga utotoni ni muhimu sana” Amesema Dkt.Gwajina.
Katika hatua nyengine, amesema kuwa ni muhimu pia kwa kina mama wajawazito kupata chanjo ya pepopunda ili kujikinga wao wenyewe na watoto wao wanaozaliwa.
Pamoja na kwamba kuna maendeleo mazuri ya utoaji chanjo kwa watoto katika miaka iliyopita,amesema ipo haja sasa kuanza kuvuka kutoka asilimia 90 hadi kufikia asilimia 100 ya upatikanaji wa Chanjo ili kuendelea kuokoa kizazi dhidi ya magonjwa.
Hata hivyo, amewataka wazazi na walezi wengine kuhakikisha wanafahamu sababu za umuhimu wa chanjo, ratiba ya chanjo inayotumika na mahali chanjo inakotolewa kwa watoto.
Dkt. Gwajima, ametoa wito kwa Wazazi wote au walezi wengine kuhakikisha kwamba wanazingatia ushauri wa mtaalamu wa afya kuhusu muda wa kukamilisha chanjo zinazohitajika.
Miongoni wa magonjwa mbalimbali yanayotolewa chanjo ni pamoja na surua na rubella,saratani ya shingo ya kizazi, kifua kikuu,kifaduro,kuharisha, nimonia, dondakoo,pepopunda,hoama ya ini, ulemavu wa ngozikama vile miguu au mikono au vyote kwa pamoja.
Katika Uzinduzi wa Chanjo Kitaifa, kauli mbiu ya mwaka huu 2021 inasema 'CHANJO HUTUWEKA PAMOJA, KAPATE CHANJO'.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa