KATIKA kuhakikisha watoto wanapata huduma za malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali kadiri ya taratibu za serikali , Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Manispaa ya Morogoro, Hamisa Kagambo,amewataka Wamiliki kukamilisha taratibu za usajili ili Vituo hivyo visajiliwe.
Akizungumza na wamiliki wa vituo vya makuzi na malezi kwa watoto wachanga na watoto wadogo,Kagambo, amesema kikao hicho, kina lengo la kusaidia uboreshaji wa huduma kwa watoto vituoni ikiwepo wamiliki kuendelea kufanya usajili wa vituo, kwani kwa kufanya hivyo kunaongezea thamani vituo hivyo na kuvifanya vitambulike rasmi kisheria.
Kagambo amesema, watoto kuwepo katika vituo hivyo kunasaidia ulinzi na usalama wa watoto, kuwepo kwa ujifunzaji wa awali kwa watoto na wazazi /walezi wanapata muda wa kufanya shughuli za kiuchumi.
Amesema usajili wa vituo hivyo ni bure kwani sheria ya mtoto namba 21 ya Mwaka 2009 kifungu cha 147 mpaka 152 na kanuni za watoto imetoa ufafanuzi kuhusu vituo vya kulelea watoto wadogo na watoto wachanga mchana na imeeleza taratibu za kufuata wakati wa kufungua vituo vya makuzi na malezi kuwa na vigezo vinavyohitajika.
" Manispaa ya Morogoro tuna jumla ya vituo 103 vinavyojulikana na ustawi wa jamii kati ya hivyo vimesajiliwa vituo 25 na vituo 5 vipo katika mchakato , hivyo ni vema kwa kila anaeanzisha vituo avisajili kwanza kwaajili ya kumlinda mtoto" Amesema Kagambo.
Naye, Mwenyekiti wa umoja wa wamiliki wa day care centers -Manispaa ya Morogoro (UWADAMO), Clarence Burchard Mkwama ambaye ndiye mmiliki wa Mary Children Day Care Sabasaba, ameipongeza idara ya Ustawi wa jamii kwa kusimamia UWADAMO na kuepelekea kuongeza uelewa kwao na kuanza kufanya mabadiliko chanya ya kutoa huduma za vituo kwa watoto na kuwepo na umoja huo utawasaidia kujadiliana na kupeana uzoefu katika eneo la huduma vituoni.
Upande wa Katibu wa UWADAMO, Bi. Mary Kessy,ambaye ndiye mmiliki wa St.Maria Consolata SUA, amesema serikali na wadau wasichoke waendelee na jitihada hizo na ikiwezekana kutoa mafunzo hadi kwa wazazi/walezi yawafikie ingawaje pia wao kama wamiliki na walezi vituoni watasaidia kutoa elimu ya malezi kwa wazazi/ walezi katika vituo.
Kwa upande wa Mwakilishi wa wamiliki kutoka Hittler Day Care , ameushukuru Uongozi wa UWADAMO, kwa kushirikiana na Manispaa ya Morogoro katika kutoa elimu na kupelekea kusaidia uundaji wa umoja wa wamiliki wa day care centers -Manispaa ya Morogoro ambapo Umoja huo umekuwa msaada wa kuongeza ujuzi kwa wamiliki na walezi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa