KAMATI ya Fedha na Uongozi Halmashauri ya Manispaa yav Morogoro leo Novemba 14, 2019, imefanya ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa ndani ya manispaa, ikiwemo mradi wa Ujenzi wa Soko kuu la kisasa Kata ya Mji Mkuu, pamoja na mradi wa Ujenzi wa Stendi mpya ya Daladala iliyopo Kata ya Mafiga.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema lengo la kutembelea miradi hiyo ni pamoja na kuangalia maendeleo ya miradi hiyo ilipoishia na inavyoendelea.
Aidha, Meya Kihanga, amesema katika ziara hiyo wamebaini kutokuwepo na kasi nzuri ya ujenzi japo maendeleo yake yanaridhisha, hivyo ametoa agizo kwa wakandarasi wanaosimamia miradi hiyo wafanye kazi usiku na mchana ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kuwahudumia wananchi.
Katika upande wa mradi wa kimkakati uliopatiwa ruzuku na Serikali kuu, Mhe Kihanga, amemtaka mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za kiuchumi na kijamii.
Amesema matarajio yake katika mradi huo ni kwamba hadi kufikia Desemba 31 , mwaka huu 2019 , mradi huo utakuwa umekamilika.
Amesema mradi huo pindi utakapokamilika utawahudumia zaidi ya wafanyabiashara 1500, huku kipaumbele cha kupewa maeneo ya biashara kitatolewa kwa wafanyabiashara waliokuwa wanafanya biashara awali kabla ya soko la zamani kuvunjwa.
" Mhandisi tunakwama wapi? unajua wakati Naibu Waziri wa fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, alipofanya ziara hapa tulikuwa katika kasi kubwa sana, nashangaa sasa hivi kasi ya ujenzi imepungua, sasa hebu tushirikiane Mkandarasi, mtaalamu mshauri wa mradi pamoja na Manispaa tuwe kitu kimoja , tunapo kwama tuambiane na kama kuna shida ya fedha ziombeni kwani pesa zipo zinatusubiria sisi na ikifika desemba 31 hizi fedha zitaondoka na tutazikosa , sitaki tuzikose maana zikiondoka nyinyi wakandarasi mtakosa fedha na sisi tutakosa fedha na tutakuwa tumekwamisha huu mradi unaotegemeawa kutoa huduma kubwa na kuingizia pato taifa pamoja na Manispaa yetu" Amesema Mhe. Kihanga
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema wataendelea na ziara za kutembelea miradi hiyo mara kwa mara kwani miradi hiyo imetengwa kwa lengo la kuifanya mamlaka za Serikali za Mitaa za Manispaa ya Morogoro ziweze kujitegemea kimapato.
Aidha amesema mradi huo utagharimu Shilingi Bilioni 17,ambapo pindi mradi huo utakapokamilika Halmashauri inategemea kukusanya takribani kiasi cha Shilingi Bilioni 2.7 kwa mwaka hivyo itapunguza kutegemea ruzuku toka Serikali kuu.
Licha ya kuridhishwa na hatua za mradi huo iliyofikiwa katika utekelezaji aliwataka wale wote wanaosimamia mradi huo kuzidisha kasi ya ujenzi, na kuona mkandarasi anakuwa site masaa ishirini na nne kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kuzuia upotevu wa fedha za wanyonge zinazotekeleza mradi huo.
Kwa upande wa Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Eng. Juma Gwisu, amesema ujenzi huo mpaka sasa umefikia asilimia 75%, na wanatarajia kukamilisha mwishoni mwa mwaka huu Desemba 31.
Mwenyekititi wa Mipango Miji na Diwani wa Kata ya Mwembesongo, Ally Kalungwana , amesema wao kama Kamati ya fedha na uongozi, hawatachoka kufanya ziara hizo kwani kufanya ziara hizo kunasaidia miradi mingi kwenda kwa kasi
Naye Kelvin Chacha, msimamizi wa mradi, amesema kuchelewa na kusua sua kwa mradi huo kumetokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi ambazo ni kuwepo kwa mtandao wa maji taka ,uwepo wa wingi wa maji eneo la maradi (High table) uvunjaji wa misingi ya majengo ya soko la zamani, pamoja na mvua zilizonyesha kipindi cha hivi karibuni.
Katika hatua nyengine, Mhandisi wa Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya Nadra Engineering Construction Company Ltd, Charles Richard, amesema ujenzi huo utakuwa na Maduka 304, Meza 900, maeneo makubwa 16 ya kupangishwa kwa mita za mraba (benki, maduka makubwa na ofisi ) maegesho ya magari makubwa 5 ya mizigo kwa pamoja, maegesho ya magari madogo 143 kwa pamoja, vyoo, migahawa, stoo 36 za mitumba, bucha pamoja na eneo la kuchinjia kuku.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa