HALMSHAURI ya Manispaa ya Temeke imeipongeza Manispaa ya Morogoro kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ikiwamo mradi wa Soko Kuu la Kisasa. pamoja na Stendi ya mabasi Msamvu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari , Oktoba 15/2021 , Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke , ambaye ndiye kiongozi wa msafara, Mhe. Abdallah Mtinika amesema kasi ya miradi ya maendeleo ya Manispaa ya Morogoro imewafurahisha hivyo amelitaka Baraza la Madiwani Manispaa ya Temeke kuhakikisha wanapo rudi nyumbani waanze kufanyia kazi kwa kile walichojifunza.
Amesema kuwa, Manispaa ya Morogoro inahitaji kupongezwa sana kwani wamepiga hatua kubwa huku wakionesha thamani ya fedha katika miradi na wamekuwa mfano wa kuigwa hususani katika miradi hiyo na kuifanya manispaa kuongeza miradi mingine katika pato lao la ndani.
Mhe. Mtinika , amefurahishwa zaidi jinsi Manispaa hiyo ilivyoweka vipaumbele hususani katika kuwahamisha wafanyabiashara kwa maridhiano na kuwapa kipaumbele mara baada ya kukamilika kwa mradi huo.
Aidha, amefurahishwa zaidi kuona Watu wenye uhitaji maalumu wametengewa maeneo yao maalumu, jambo ambalo linalenga kuleta usawa kwa wote na kuendeleza adhima ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuwaendeleza walemavu , wakina Mama pamoja na vijana.
"'Niwapongeze viongozi wa Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani na Wataalamu, kazi inaonekana , kwakweli katika miradi yenu kuna vitu vingi tumejifunza, sisi kwetu tuna miradi mingi lakini tumejifunza jinsi ya kuendesha mradi wa Soko na tukirudi tutakwenda kukaa na wafanyabiashara kuona jinsi gani tutawasogeza kwa maridhiano kujenga soko nje ya mji haitakuwa biashara nzuri kwetu bora tujenge katikati ya mji ili tuweze kupata mapato, kingine katika mradi wa stendi ya Msamvu tumeona wakaguzi wa kimataifa wanavyofanya kazi yao kwakweli inaonesha ni jinsi gani Manispaa yenu mlivyo karibu na Serikali pamoja na Chama Tawala CCM" Amesema Mhe. Mtinika.
"Ukiangalia Manispaa yetu ya Temeke , tunataka kuibua miradi mikubwa lakini tunahitaji kukusanya kodi katika miradi hiyo, hivyo lengo letu kubwa kuja hapa ni kuona namna gani tutapata uzoefu na kujua wenzetu wanatumia aina gani ya ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa miradi ili nasisi tuweze kufanya kama wanavyofanya wao japo sisi mapato yetu makubwa lakini kujifunza hakuna mwisho hata mtoto anaweza kujifunza kwa mkubwa " Ameongeza Mhe. Mtinika .
Hata hivyo, amesema watamshauri Mkurugenzi pamoja na Baraza la Madiwani la Halmshauri ya Manispaa ya Morogoro , kuhakikisha mara baada ya kukamilika kwa miradi ya maendeleo waweke uongozi mzuri ambao wataamua katika Baraza lao na utakaokuwa unauwezo wa kukusanya fedha ili Manispaa iweze kuendesha miradi mingine.
Amesema siku zote katika kuhitaji maendeleo lazima ujifunze kwa mwenzako maana rasilimali pesa inakuwa ndogo kuliko idadi ya watu, hivyo wamejifunza jinsi ya kuendesha miradi vizuri, isije tena ikwawa wameibua miradi,harafu miradi hiyo ukaleta migogoro na kutokuwa na tija kitu ambacho hakitawasaidia katika kufikia malengo yao ya kukusanya kodi.
Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, , ameipongeza Manispaa ya Temeke kwa kujitolea kuja kujifunza namna ya kuendesha miradi na jinsi ukusanyaji wa mapato.
Mhe. Kihanga, amesema kujifunza sio dhambi hivyo wataendeleza ushirikiano huo pindi pale watakavyohitajika kufanya hivyo kwa Ustawi wa Maendeleo ya Tanzania na Wananchi kwa Ujumla.
Amesema kuwa kujifunza ni njia ya kupata maendeleo zaidi ,hivyo kwa kupitia mafunzo hayo Manispaa ya Temeke watanufaika sana na wataimarisha mifumo ya kodi na kuiletea Manispaa yao Mendeleo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Michael Waluse, amesema kuwa , Manispaa ya Morogoro ipo chini kimapato ukilinganisha na Manispaa nyengine za Mjini kama kwenye Majiji makubwa , lakini wanajitahidi sana kufuatilia vyanzo vya mapato , amewahahakishia ushirikiano na kunufaika na lengo la ziara yao yenye kulenga kuwajengea uzoefu na kujua mbinu wanazotumia za ukusanyaji wa mapato.
" Kweli tumewapokea ndugu zetu wa Manispaa ya Temeke kutoka Jiji la Dar Es Salaam, kwa ajili ya kuja kujifunza hapa kwetu, matumaini yangu ni kwamba tangia walivyokuja ni tofauti na sasa baada ya kuondoka, lakini tunachowaambia mafanikio yetu ni kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha za miradi , hivyo tunakusanya fedha nyingi lakini hizi fedha tunazipeleka kwenye miradi ya wananchi na miradi hiyo inaonekana, lakini Manispaa ya Morogoro tumekuwa na miradi mikubwa matarajio yetu baada ya miradi hii kukamilika tutakusanya pesa na tutazielekeza katika kuibua miradi mengine ya maendeleo"Amesema Waluse.
Waluse, amesema ili kufikia lengo katika ukusanyaji wa kodi ni lazima uheshimu misingi ya matumizi mazuri ya pesa pamoja na kuwekeza katika miradi ya wananchi.
Naye Mbunge wa Jimbo la Temeke, Mhe. Dorothy Kilave, ameipongeza Manispaa ya Morogoro kwa hatua nzuri za usimamizi wa Soko lakini katika mfumo mzima wa kuwapanga Machinga na kuwaweka sehemu moja.
"Wenzetu wamefanya jambo kubwa sana, tuna cha kujifunza hapa, na sisi tukirudi tutachukua njia zote nzuri ambazo wenzetu wa Manispaa ya Morogoro wamezitumia kwanza kusimamia Soko kubwa kama hili na jinsi walivyoweza kuwapanga Machinga katika mpangilio mzuri, niupongeze Uongozi wa Mkoa, Wilaya ya Morogoro na Manispaa kwa hatua kubwa za kuwawekea Machinga Mazingira rafiki ya kuifanyia biashara zao za kujiingizia kipato " Amesema Mhe. Kilave.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa