Mwenyekiti wa Kamati ya Mipangomiji na Mazingira Manispaa ya Morogoro Mhe.Amiri J.Nondo leo tarehe 12/04/2018 amezindua rasmi kampeni ya upandaji miti.Uzinduzi huo umefanyika katika shule ya Msingi Mkundi.
Mhe. Nondo akizungumza wakati wa zoezi hilo amesema kwa kuzingatia waraka wa Serikali,Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa wiki hii ya upandaji miti ambayo uzinduzi wake umefanyika leo jumla ya miche 5000 ya miti mbalimbali ikiwemo mitiki,mikongo na migrivelia itapandwa katika kata ya Mlimani(miti 1,000) na kata ya Mkundi (miti 4000).
Mhe. Nondo amesema kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu inayosema "Tanzania ya kijani inawezekana,Panda miti kwa Maendeleo ya Viwanda" hivyo upandaji miti utapendeza sana kwa maendeleo ya viwanda iwapo mazingira yatatunzwa na kuweza kuwavutia wawekezaji mbalimbali wa viwanda vikubwa , vya kati na vidogo ,lakini pia kwenye biashara za mahoteli,nyumba za kulala wageni,maduka,masoko na hivyo kuchangia mapato katika Manispaa ya Morogoro.
Aidha ameeleza kampeni ya upandaji miti iliyozinduliwa iwe endelevu na iwashirikishe wananchi wote wa Manispaa ya Morogoro katika maeneo wanayoishi,pamoja na sekta zote binafsi ili kutoa fursa walizonazo katika kupanda miti kwa wingi.
"Uzinduzi wa upandaji miti uende sambamba na udhibiti wa ongezeko la watu lisilowiana na mahitaji ili kudhibiti ongezeko la shughuli za kibinadamu zinazochangia uchomaji moto hovyo,ukataji wa misitu kwaajili ya kilimo kisichokuwa endelevu,ujenzi wa makazi,nishati kama mkaa,kuni na mbao na uwindaji wa wanyama"ameeleza Mhe. Nondo.
Aidha ameshauri jitihada zaidi ziongezeke ili kunusuru hali ya uharibifu a maliasili na mazingira unaoendelea nchini ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.Pia amesisitiza suala la uhifadhi wa uoto wa asili na mapori ya akiba yaliyopo kwenye Manispaa yetu lipewe umuhimu unaostahili kwa mfano maeneo ya hifadhi yaliyopo kwenye milima ya Uluguru,eneo la Nguru ya Ndege,na eneo la msitu wa Mindu.
Naye Diwani wa Kata ya Mkundi Mhe Hilda Benedict ametoa shukrani kwa kuteua kata hiyo kufanyia uzinduzi na kusisitiza wananchi kuitunza na kuithamini miti hiyo itakayopandwa.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa