MKUU wa Mkoa wa Morogoro Mh. Martine Shigela, amewataka Wazazi na walezi Mkoa wa Morogoro kuendelea kuwekeza katika elimu kwa manufaa ya watoto wao na kwa maisha ya badae na Taifa kwa ujumla.
Hayo ameyazungumza Juni 01/2022 katika Mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi wa Kata ya Kihonda Manispaa ya Morogoro mkutano uliofanyika eneo la Ofisi ya Kata Kihonda.
Akizungumza na Wananchi hao, RC Shigela, amesema Taifa lolote ili liweze kupata maendeleo Wananchi wake lazima wasome na kupata elimu iliyo bora sio bora elimu.
" Serikali yetu ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kipaumbele chake ni elimu na ndio maana imewekeza sana katika Sekta ya Elimu, nawaomba wazazi na walezi kufuatilia maendeleo ya watoto wenu katika sekta ya elimu na kuwalea watoto katika misingi ili wawe na maadili waweze kufanya vizuri darasani na katika mitihani yao ya Wilaya, Mkoa na ngazi ya Taifa na sio kuwaachia waalimu katika malezi jambo ambalo sio jema katika misingi ya kuwalea watoto" Amesema RC Shigela.
RC Shigela, amewataka Wananchi wa Mkoa wa Morogoro kuunga mkono juhudi za Serikali juu ya Sera ya elimu bila malipo kwa kuwasomesha watoto na kufatilia maendeleo yao kitaaluma.
" Wanafunzi hawa ndio madaktari wa kesho na Wabunge na mawaziri tuwalinde watoto wetu na kuwasomesha ili waweze kuwa na nidhamu" Ameongeza RC Shigela.
Wakati huohuo, RC Shigela, amewataka Wanawake ,Vijana na Watu Wenye Ulemavu kuchangamkia fursa za Serikali kwa kukopa mikopo ya Serikali ambayo inatolewa ngazi ya Halmashauri ili wafanye biashara na Kupata fedha za kulipa ada kwa ajili ya elimu.
Hata hivyo, amesema Mkoa wa Morogoro unapokea jumla ya shilingi Bilioni 1 kila mwezi fedha ambazo zinaelekezwa katika Shule za Msingi na Sekondari kwa ajili ya elimu bure bila malipo.
Mwisho, RC Shigela, amepiga marufuku michango isiyo ya lazima shuleni huku akisema michango yote inayotakiwa kupitishwa ipitie kwa Mkuu wa Wilaya ili iweze kupatiwa kibali cha mchango.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa