WANAFUNZI wa kike wa vyuo vikuu na vya Kati Mkoa wa Morogoro wametakiwa kujitambua na kufahamu wajibu wao kwa jamii inayowazunguka na kujiepusha na vishawishi vikiwemo vya ngono na kujikomboa kifikra, kiutamaduni na kiuchumi.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Pili Kitwana, Julai 31/2021 akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigela, katika sherehe ya Mabinti iliyoandaliwa na Taasisi binafsi ya Wanawake ya Ladies Talk Tanzania Initiatives iliyo chini ya Mkurugenzi wake Salome Sengo kwenye eneo la Chuo Kikuu cha Jordan Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kitwana amewataka wanawake hao na Mabinti kujua thamani yao na kuepuka kutumiwa vibaya na kushinda majaribu ya watu wanaotaka kuivuruga safari yao ya maisha.
Kitwana, alisema kila mtu amepewa karama za kumuwezesha kufikia wito wa kutimiza ndoto zake ili kuweza kufanikisha hayo hana budi kujitambua, kuvitunza na kuvilea vipawa na karama zake na kuyakubali mapungufu yake katika kutimiza azma zake.
“Kataa kabisa mawazo ya kukatisha tamaa kwani hofu kama ilivyo furaha huambukiza, jaribu kuwaepuka marafiki wenye mawazo ya kukatisha tamaa kwani hao ndiyo maadui wakubwa wa maisha yako na wa kukukwamisha kufikia malengo yako, lakini kikubwa sana upendo wa dhati kabisa mkipendana kutoka moyoni mtafanikiwa sana ” alisema Kitwana .
“Kuna wakati inawezekana ukawa na hamu ya kuona malengo yako yanatimia mara moja ukweli ni kwamba hamu yako ya kuleta mabadiliko ya haraka yanaweza kukuletea madhara makubwa kuliko faida na hapa ndipo mabinti wengi huharibikiwa kwa sababu wanakosa subira na hivyo kufanya mambo yao kinyume na utaratibu na malengo,” aliasa Kitwana.
Aliwahimiza wanafunzi hao kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika vyuo vyao kwa kufanya hivyo watajiwekea mazingira mazuri ya kuwa viongozi wa baadaye pindi watakapomaliza masomo.
“Wanawake tuna nafasi ya pekee ya uongozi kwani sisi ndio wazazi na walezi tunaokabiliwa na changamoto nyingi,hata Rais wetu wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan ni mwanamke ambaye kabisa mnaona makubwa anayoyafanya katika Taifa letu, hivyo basi sisi tuna mchango wa pekee katika kutatua changamoto hizo lakini tutaweza kufanya hivyo kama tutaingia katika ngazi ya maamuzi jambo la muhimu ni kupendana na kuungana katika mambo ya maendeleo kwa ajili ya maslahi yetu kama wanawake,” alisisitiza Kitwana.
Mwisho Kitwana, alikubali kuwa Mlezi wa Ladies Talk Tanzania Initiatives na kuahidi kiasi cha Shilingi Milioni 1 katika kuiwezesha Taasisi hiyo kuendesha majukumu yake na kuendelea kuwatafutia wadau mbalimbali na kuwakaribisha katika kuchangamkia mkopo wa Manispaa wa asilimia 10.
Naye Mkurugenzi wa Ladies Talk Tanzania Initiatives, Salome Sengo, alisema katika maisha suala la kujitambua ni la muhimu kwakuwa wanafunzi wengi wa elimu ya juu wanasoma bila ya kuwa na malengo hali inayosababishwa na kutojitambua.
“Changamoto zinazomkabili mtoto wa kike ni nyingi baadhi ni kutokuwa na elimu ya afya ya uzazi na jinsia jambo ambalo limesababisha wasichana wengi kujihusisha katika mahusiano yasiyo salama, dhana potofu ambayo imejengeka katika jamii kwamba wanawake hawawezi kuwa viongozi kiasi cha kuwaathiri hata watoto wa kike wenye uwezo wa kuongoza,” alisema Sengo .
Alisema sera nyingi za nchi zimemsahau mtoto wa kike katika mambo yanayomuhusu na hivyo kumfanya aonekane duni kwenye jamii.
Wanafunzi hao pia waliiomba serikali itazame upya sera ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu hasa wasichana kwakuwa wengi wao hawakidhi vigezo vya kupewa mikopo na wanahitaji kusoma hivyo wanafunzi wanaotoka katika familia zenye uwezo duni kiuchumi kushindwa kuendelea na masomo.
Sherehe hiyo ya wanawake na mabinti iliandaliwa Taasisi ya Ladies Talk Tanzania Initiatives kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Jordan.
Sherehe hiyo ya Wanawake na Mabinti ilihudhuriwa na jumla ya Mabinti 170 ambao walipendeza kwa mavazi na
Miongoni mwa wafadhili wakubwa wa sherehe hiyo ni pamoja na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Mhe. Norah Mzeru, Cate Hotel , Eli's Catering and Fashion, pamoja na Suzie Make up Glam.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa