Watendaji wa Kata na Mitaa Halmshauri ya Manispaa ya Morogoro, wametakiwa kushughulikia malalamiko na migogoro iliyoko katika maeneo yao ili iwe chachu ya maendeleo na kuleta mabadiliko chanya kwa Jamii.
Hayo yamezungumzwa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Serikali za Mitaa Mkoa wa Morogoro, Bi. Erica Yegele kwenye kikao kazi cha kufunga mwaka kilichofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Manispaa Morogoro Desemba 31,2019.
Amesema kuwa Watendaji wanatakiwa kuwasilisha mihutasari ya vikao vyao kwa wakati , ikiwamo kuzingatia muda, nyakati na kutoa ripoti zenye uhalisia.
Ametoa agizo kwa kila Mtendaji kuwa na daftari la rejesta za malalamiko na hatua walizochukua baada ya kupokea malalamiko ili kurahisisha utendaji kazi kwa kutoa huduma bora kwa Wananchi wao.
'Nawaomba watendaji mfanye kazi kwa bidii, hali si shwari katika maeneo yetu, pia suala la usalama bado hafifu mfano kata ya Mafiga , niwaombe wakusanyeni hao vibaka na kuwatafutia mradi wa pamoja nipo tayari kutoa hata pesa zangu za mfukoni ili usalama wa wananchi uimarike" Amesema Bi Yegela.
Katika hatua nyingine amelalamikia kushuka kwa nidhamu shuleni, hivyo amewataka Watendaji kujenga utaratibu wa kuzifikia shule na kuzungumza na Wanafunzi pamoja na waalimu ili kujenga mazingira mazuri na rafiki na nidhamu za wanafunzi wa Manispaa ya Morogoro.
Aidha amesema ni wakati wa Watendaji kushiriki kikamilifu katika suala zima la usafi na kusimamia vyema vikundi vya kufanya usafi kwani hali ya usafi katika baadhi ya maeneo hairidhishi.
Pia amesema Manispaa ya Morogoro ipo chini kimapato, hivyo Watendaji washirikiane katika kusimamia vyema vyanzo vya mapato na kuifanya Halmshauri kujiendesha yenyewe bila ya kutegemea fedha kutoka kwa wafadhili na Serikali kuu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa