Mratibu wa Wazee wa Manispaa ya Morogoro, Bi. Hamisa Kagambo, ameyataka mabaraza ya wazee kuendelea kushirikiana na Serikali na kuwa na imani nayo kwani Serikali ipo pamoja nao katika kuhakikisha inatekeleza afua mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa wazee.
“Manispaa ya Morogoro inaendelea na juhudi za kuhakikisha Ustawi wa Wazee unaimarika ikiwemo kuimarisha mifumo ili wazee wapate huduma za kijamii kama Afya, ulinzi, usalama na matunzo kwenye makazi ya wazee” alieleza Kagambo.
Kagambo amesema hayo tarehe 19.10.2023 katika sherehe ya maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, iliyofanyika katika ukumbi wa Double M- Mazimbu ambapo jumla ya wazee 100 wameweza kupimwa magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari na presha.
Naye Mkurugenzi wa Asasi isiyo ya Kiserikali ya Woman Of Substance, Bi. Mariam Mlembele, ametoa wito kwa wazee kuwaandaa na kuwalea vijana kwa ajili ya maisha ya uzeeni ikiwa ni pamoja na kukemea vitendo vyote vilivyo kinyume na maadili ya kitanzania.
"Katika zama hizi tunahitaji zaidi Wazee waendelee kufanya mengi ili kuambukiza vizazi vipya tabia njema na kuwezesha nao kufikia uzee ulio mwema lakini cha kusikitisha hivi karibuni kumekuwa na Wazee wanaoripotiwa kufanya matukio ya ajabu yasiyolingana na umri wao mfano kubaka na kulawiti watoto, kuwaoza watoto wadogo na kupandikiza imani mbaya" Ameongeza Mlembele.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Kata ya Mazimbu, Isack Wella, amesema kuwa ili wazee wajikwamue kiuchumi katika baraza lao wamepanga kuwa na miradi ya maturubai, viti vya plastiki, na Mahema ambavyo vyote vina gharama ya Shilingi Milioni 1 laki 6.
Wella, amesema Kata ya Mazimbu ina Wazee 700 katika Mitaa yote 7 ambapo kati ya wazee hao, wazee 402 ndio wameweza kupatiwa Bima ya Afya ya Msamaha wa Matibabu.
Nao wazee waliohudhuria katika maadhimisho hayo, wameiomba Serikali kupitia Halmashauri zao itunge sheria ndogondogo ili kudhibiti ukiukwaji wa maadili katika jamii, na wameiomba Serikali katika madhimisho ya mwaka 2024 iongeze huduma ya upimaji macho kwani asilimia kubwa ya wazee wanasumbuliwa na matatizo ya macho.
Akitoa salamu za Baraza la Manispaa la Wazee, Katibu wa Baraza hilo la Manispaa, Dkt.Basil Anga,amelipongeza Baraza la Mazimbu kwa maadhimisho mazuri huku akiwaomba Viongozi wa Mabaraza ya Kata na Mitaa ambao wanachangamoto za Uongozi wajitoe na kupisha Viongozi wengine kuongoza.
Naye Mkurugenzi wa Shirika la kuhudumia Wazee Mkoa wa Morogoro, MOREPEO , Samson Msemembo, amesema MOREPEO ni Shirika ambalo lina shughulika na Changamoto za Wazee Mkoa wa Morogoro pamoja na kuwasemea wazee wote katika ngazi mbalimbali za Mitaa, Wilaya, Mkoa hadi Taifa.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa