WAZIRI wa Mambo ya ndani ya nchi Dk Mwigulu Nchemba,amewaonya watendaji wa mitaa na kata ambao wanawatoza fedha wananchi katika zoezi la usajili na utambuzi wa watu linalofanywa na mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) kuacha mara moja na wale watakaobainika watafukuzwa kazi.
Waziri Dk Nchemba alitoa agizo hilo baada ya kuzindua zoezi la usajili na utambuzi wa watu mkoani Morogoro linalofanywa na Nida na kuwagiza viongozi wa mkoa wa Morogoro kusimamia kwa karibu zoezi hilo na kuwabaini mara moja watendaji wanaowatoza wananchi fedha .
Alisema kuwa Serikali imegharamia kila kitu katika zoezi hilo na hakuna mwananchi anayepaswa kutozwa kiasi chochote cha fedha na kutaka kila mwananchi kujitokeza kujisajili ili kupata vitambulisho hivyo na kuwasisitizia viongozi hao kuhakikisha hakuna mtu ambaye si raia anayepenya na kupewa kitambulisho cha taifa.
Waziri Nchemba aliwahakikishia wananchi wa mkoa kuwa wizara imejipanga kwa kuhakikisha kwamba ifikapo Desemba 2018 wananchi wote hapa nchini wenye umri wa miaka 18 na kuendelea wawe wameshasajiliwa na kupata namba za utambulisho.
Alisema kuwa dhamira ya Serikali katika zoezi hilo ni kuhakikisha wananchi wanatumia vitambulisho vya Taifa kwa matumizi mbalimbali na kusisitiza kwamba vitambulisho hivyo vinatolewa bure.
Awali Akisoma taarifa ya utendaji kazi wa mamalaka hiyo ya vitambulisho vya Taifa (Nida) Kaimu mkurugezi mkuu wa Nida Andrew Massawe alisema kuwa tayari vifaa zikiwemo mashine 200 zimesambazwa ili kukidhi mahitaji ya usajili na kuhakikisha ifikapo Aprili 30 mwaka huu zoezi ile liwe limekamilika.
Kaimu mkurugenzi huyo alisema kuwa Nida imetoa ajira za muda mfupi kwa wananchi 200 na kufungua ofisi kwenye wilaya zote ambapo jumla ya maafisa 23 wa kudumu kutoka Nida wamegawanywa kwenye wilaya zote kwa lengo la kusaidiana na watendaji wa wengine kuhakikisha zoezi linafanikiwa.
Massawe alieleza baadhi ya faida za kuwa na kitambulisho cha taifa kuwa ni pamoja na kuweza kupata huduma kirahisi za afya, elimu na fedha na za kiulinzi na usalama.
Katika hatua nyingine Kaimu mkurugenzi huyo aliitaja mikoa ambayo imefanya vizuri katika zoezi hilo la usajili na utambuzi kuwa ni pamoja na Iringa, Mara, Simiyu,Arusha, Geita, Mwanza, Ruvuma, Kilimanjaro na Lindi ambapo alisema kuwa mafanikio hayo yalitokana na uongozi madhubuti wa mikoa hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa mkuu wa mkoa wa Morogoro Dk Stephen Kebwe alisema kuwa jumla ya wananchi 961,309 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea watasajiliwa hata hivyo alisema kuwa katika kipindi hiki cha kilimo kinaweza kuwa changamoto kwa wananchi kujitokeza kwani wengi wako mashambani.
Dk Kebwe aliwataka viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kuhamasisha wananchi kujitokeza kwenye zoezi hilo huku akitoa onyo kwa baadhi ya wanasiasa kutopotosha na kubeza dhamira ya zoezi na kwamba yeyote atakayebainika kukwamisha zoezi hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa