Taasisi isiyo ya Kiserikali ya WEZEESHA MABADILIKO chini ya Mkurugenzi wake. Dr. Lusako Mwakiluma,imeikabidhi Manispaa ya Morogoro Choo cha Mtoto wa Kike ilichokijenga katika Shule ya Sekondari Uluguru.
Tukio hilo la makabidhiano ya choo limefanyika hivi karibuni ambapo katika makabidhiano kilipokelewa na mwakilishi wa Mkurugenzi kutoka idara ya elimu Msingi, Bi.Leah Selemani.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi choo hicho, Mkurugenzi wa WEZESHA MABADILIKO, Dr. Lusako, amesema kwa kuwa wanawake wengi wamekuwa na changamoto nyingi katika mabadiliko ya kimwili hivyo wameona kujenga Choo cha Mtoto wa kike itakuwa ni suluhisho la kuwaondolea adha wanafunzi wa kike wanapoingia katika hedhi.
Dr. Lusako,amesema kuwa tafiti zinaonesha kuwa mtoto wa kike anakosa masomo siku 4 hadi 5 kila mwezi kutokana na ukosefu wa huduma ya vyoo bora na maji salama na safi shuleni ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini mkataba wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Miongoni mwa malengo hayo ni lile lengo namba 4: linalohamasisha kuhusu Elimu Bora, Lengo la 5: linalo hamasisha juu ya Usawa wa Kijinsi na lengo namba 6: kuhusu Maji Safi na Salama.
“Huu ni mwanzo tu bado tuna malengo ya kusaidia na shule nyingine , tunataka choo hiki kiwe cha mfano katika Manispaa yetu ya Morogoro , tuliona kuna Choo Tubuyu Sekondari lakini kuna kingine hakijaisha pale Kihonda Sekondari, sisi baada ya kuguswa na jitihada hizi, tumeona nasisi tuunge mkono jitihada za Manispaa yetu kwa kuwajengea Choo hiki cha Kisasa ili kuhakikisha mtoto wa kike anawekewa mazingira rafiki anapokuwa shuleni ili aweze kuhudhuria siku za masomo kwa ukamilifu kama ilivyokuwa kwa mtoto wa kiume kwani “Ukimkomboa mtoto wa kike umekomboa Taifa zima” Ameongeza Dr. Lusako.
Aidha, amesema kuguswa kwao katika ujenzi wa Vyoo vya Mtoto wa kike imetokana na changamoto zinazoendelea kuwakabili wanafunzi kukosa vyoo bora na maji salama na safi shuleni. Tatizo hili linawaathiri watoto wa kike zaidi kwani wanashindwa kujistiri hasa wanapokuwa katika siku zao za hedhi katika mazingira ya shuleni.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro,ambaye pia ni afisa Taaluma Msingi, Leah Selemani, amempongeza Mkurugenzi wa WEZESHA MABADILIKO kwa kuwasaidia wanafunzi wa kike shuleni.
Amesema vyoo hivyo vitapunguza utoro kwa watoto wa kike kwani wengi wamekuwa wakishindwa kufika shule wakati wa hedhi lakini baada ya ujenzi huo utasaidia sana na wanafunzi watahudhuria shule wakiwa katika hali hiyo maana ipo sehemu salama kwao katika kujisafisha na kujilinda.
Bi. Selemani , ameowaomba Wazazi kuwahimiza watoto kwenda shule mara baada ya kupata hedhi kwani mabadiliko hayo yanazuilika wakiwa shuleni.
“Dada yetu Dr. Lusako, amefanya jambo zuri sana, sisi kama Manispaa tunampongeza sana kwa jitihada zake, hii ni mbinu nzuri sana , hiki ni choo cha 3 kwa Manispaa yetu, kimoja kipo Tubuyu Sekondari, kingine kipo Kihonda Sekondari hakijaisha na mategemeo yetu kiishe mwaka huu 2022, choo hiki kitasaidia kupunguza utoro kwa watoto wa kike wanaoingia katika siku zao (hedhi), kumekuwa na changamoto wanafunzi kubeba pedi kwenye begi na kwenda nazo shule wengine wanaenda kuomba ofisini , lakini kwa hali hii ni vigumu hata kutambua mtu yupo katika hali gani maana vifaa vyote vitakuwa chooni ni yeye kwenda na kujihudumia”Amesema Bi. Selemani.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa