ZAIDI ya Wafanyabiashara 200 kutoka makundi mbalimbali Manispaa ya Morogoro wameshiriki katika mafunzo ya utunzaji fedha yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Manispaa ya Morogoro kupitia Idara za Maendeleo ya Jamii na Viwanda,Biashara na Uwekezaji.
Mafunzo hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro na kushirikisha zaidi ya wafanyabiashara 200 kutoka maeneo mbalimbali.
Akizungunza kwa niaba ya washiriki wenzake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Soko Kuu la Chifu Kingalu, Khalid Mkunyegere,amesema kuwa elimu hiyo imekuja wakati muafaka na italeta manufaa kwa wananchi.
"Mimi kama mfanyabishara na kiongozi wa wafanyabiashara katika Soko la Chifu Kingalu, napongeza sana juhudi hizi za Serikali, elimu ya fedha inahitajika sana katika mkoa wetu kutokana na wengi wetu kufanya mambo kwa mazoea " Amesema Mkunyegere
Kwa upande wake mfanyabiashara Bi. Mwajuma Issa, amesema kuwa elimu iliyotolewa itawasaidia kutunza fedha katika taasisi rasmi, ili ziweze kuwasaidia kwa matumizi ya muda mrefu.
"Sisi tumezoea mtu ukipata hela unaziingiza kwenye matumizi zote, tena matumizi yenyewe ni ya shughuli za unyago na sherehe zingine, hali ambayo imekuwa ikizidisha umasikini kwa wananchi wengi hivyo elimu hii itatusaidia kuepukana na hilo" Amesema Bi. Mwajuma
Awali akizungumzia mafunzo hayo, Afisa Usimamizi kutoka Wizara ya fedha,Stanley Kibakaya,amesema kuwa lengo ni kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya masuala ya fedha kwa ujumla.
"Programu hii inalenga kuwafikia wananchi wengi kutoka katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Morogoro , tumeanza na Manispaa ya Morogoro na kuendelea na Wilaya nyingine ili pamoja na mambo mengine wafahamu maeneo rasmi ya kupata huduma za kifedha na namna ya kuzisimamia fedha zao kwa ajili ya kuwaletea maendeleo"Amesema Kibakaya.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa