HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro katika mapato yake ya ndani ipo mbioni kukamilisha Choo cha Mtoto wa kike chenye matundu 12 na thamani ya Shilingi Milioni 35 kilichopo Shule ya SekondariTubuyu, ikiwa na lengo la kuwasaidia wanafunzi wa kike kuweza kukamilisha haja zao kipindi cha hedhi.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Aprili 15, 2020, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, Mara baada ya kukagua mradi huo , amesema kwa kuwa wanawake wengi wamekuwa na changamoto nyingi katika mabadiliko ya kimwili wameona sasa ipo haja ya Shule zilizopo Manispaa ya Morogoro kujenga Vyoo vya Mtoto wa kike mara baada ya kilichopo kukamilika.
“Wanafunzi wengi wa kike wanachangamoto hususani katika kipindi cha siku zao za hedhi, wanapoingia katika siku zao, wengi wanashindwa kufika shule kwa hali waliyonayo, hivyo katika fedha nilizotenga kwa ajili ya elimu Sokondari , tumeona ni vyema tukawajengea vyoo hivi viwasaidie katika kujikinga na kujisafisha kipindi wanapoingia katika hedhi, niwaombe wanafunzi wote wasiwe watoro shuleni watambue hedhi sio ugonjwa bali ni mabadiliko ya mfumo wa uzazi, vyoo hivi vitakuwa na bafu maalumu litakalo kuwa na sehemu maalumu ya kutunzia vifaa vyote muhimu , ikiwemo taulo za Mtoto wa kike pamoja na kioo cha kujiangalia na sabuni kwa ajili ya kunawia na kuogea”Amesema Sheilla.
Amesema kuwa tafiti zinaonesha kuwa mtoto wa kike anakosa masomo siku 4 hadi 5 kila mwezi kutokana na ukosefu wa huduma ya vyoo bora na maji salama na safi shuleni ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini mkataba wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Miongoni mwa malengo hayo ni lile lengo namba 4: linalohamasisha kuhusu Elimu Bora, Lengo la 5: linalo hamasisha juu ya Usawa wa Kijinsi na lengo namba 6: kuhusu Maji Safi na Salama.
“Huu ni mwanzo tu, tunataka choo hiki kiwe cha mfano katika Mkoa wetu wa Morogoro, ni matumani yangu baada ya kukamilika kwa choo hiki tutaendelea na ujenzi wa vyoo vyingine ili kuhakikisha mtoto wa kike anawekewa mazingira rafiki anapokuwa shuleni ili aweze kuhudhuria siku za masomo kwa ukamilifu kama ilivyokuwa kwa mtoto wa kiume kwani “Ukimkomboa mtoto wa kike umekomboa Taifa zima” Ameongeza Sheilla.
Amesema kuwa ujenzi wa Vyoo vya Mtoto wa kike imetokana na changamoto zinazoendelea kuwakabili wanafunzi kukosa vyoo bora na maji salama na safi shuleni. Tatizo hili linawaathiri watoto wa kike zaidi kwani wanashindwa kujistiri hasa wanapokuwa katika siku zao za hedhi katika mazingira ya shuleni.
Naye Afisa Elimu wa Sekondari Manispaa ya Morogoro, Dkt. Janeth Barongo, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kwa mbinu nzuri ya kuwasaidia wanafunzi wa kike shuleni.
Amesema Vyoo hivyo vitapunguza utoro kwa watoto wa kike kwani wengi wamekuwa wakishindwa kufika shule wakati wa hedhi lakini baada ya ujenzi huo utasaidia sana na wanafunzi watahuduhuria shule wakiwa katika hali hiyo maana ipo sehemu salama kwao katika kujisafisha na kujilinda.
Ameowaomba Wazazi kuwahimiza watoto kwenda shule mara baada ya kupata hedhi kwani mabadiliko hayo yanazuilika wakiwa shuleni.
“Mkurugenzi wetu amekuja na mbinu nzuri sana, kwakweli hiki choo kitakuwa cha mfano katika Mkoa wetu wa Morogoro, ambapo kitasaidia kupunguza utoro kwa watoto wa kike wanaoingia katika siku zao (hedhi), kumekuwa na changamoto wanafunzi kubeba pedi kwenye begi na kwenda nazo shule wengine wanaenda kuomba ofisini , lakini kwa hali hii ni vigumu hata kutambua mtu yupo katika hali gani maana vifaa vyote vitakuwa chooni ni yeye kwenda na kujihudumia”Amesema Dkt.Barongo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa