Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, ndugu Ally Machela ameuambia umma wa Manispaa hiyo kwamba barabara zenye urefu wa kilomita 20.5, katika Kata za Chamwino, Tungi, Tubuyu na Kihonda zinatazamiwa kujengwa kwa kiwango cha lami, kupitia mradi wa kuboresha miji wa TACTIC.
Mkurugenzi Machela ameyasema hayo alipokuwa akizungumzia hali ya barabara za Manispaa kwa sasa, alipokuwa katika kikao na waandishi wa habari wa kituo cha Redio na Televisheni cha Abood, ambapo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiteua Manispaa ya Morogoro kuwa miongoni mwa wanufaika wa mradi wa TACTIC katika awamu hii ya kwanza ya utekelezaji wake kwani hali ya barabara za Manispaa hiyo kwa sasa ni mbaya kwa sababu kuna mitaa haipitiki na iko mjini.
“Kupitia mradi wa TACTIC barabara za lami zitakazojengwa ni barabara ya VETA Kihonda, barabara ya Tungi mpaka Star City, barabara ya Tubuyu mpaka Nanenane makaburini na barabara iliyobatizwa jina Mayele kutokana na mtetemeko wake pindi vyombo vya usafiri vinapopita juu yake huko kwenye Kata ya Chamwino.
Vilevile kupitia TACTIC, mifereji yenye urefu wa kilomita 4.4 itajengwa, ukiwemo mfereji korofi huko Mazimbu, ambao mara nyingi katika vipindi vya mvua umekuwa kero kubwa kwa wananchi wa Kata hiyo. Na mara ujenzi wa barabara hizo na mifereji hiyo utakapokamilika, tutavikabidhi kwa TARURA kwa ajili ya usimamizi zaidi” alifafanua Machela.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Machela alibainisha jitiada za Manispaa katika kuisaidia TARURA kuhakikisha Manispaa inakuwa na barabara zinazopitika, ambapo alisema katika mwaka huu, Manispaa imefungua barabara zaidi ya kilomita 120 kwenye eneo la Kiegea Kata ya Mkundi, na kujenga vivuko kwenye Kata za pembezoni kama vile Kata ya Ruhungo na sasa Kata za Bigwa na Mindu ndizo zitakazofuatia kujengewa vivuko.
Aidha, Mkurugenzi Machela amesema, mwaka huu Manispaa imetenga zaidi ya shilingi milioni 700 kwa ajili ya kununua greda ambalo italikabidhi kwa TARURA ili kuchagiza kasi ya uchongaji wa barabara za pembezoni mwa Manispaa na kuhakikisha wananchi wa Manispaa ya Morogoro wanakuwa na barabara nzuri zinazopitika wakati wote.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa