WANANCHI wa Manispaa ya Morogoro wametakiwa kujenga utamaduni wa kusafisha mazingira yao mara kwa mara ili kuepuka madhara yanayotokana na uchafuzi wa mazingira.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha usafishaji Manispaa ya Morogoro,Rumisha Kisanga, ikiwa ni mwisho wa mwezi wa usafi pamoja na maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayotarajiwa kufanyika Juni 05-2025.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro,Kisanga, amewataka wakazi wa Manispaa ya Morogoro kusafisha mara kwa mara mazingira yao ya nyumbani pamoja na maeneo wanapofanyia shughuli zao huku akiwataka wananchi kufanya usafi wa pamoja kila siku ya Jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Mazingira, Dauson Jeremia, amewataka wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi katika maeneo yao mara kwa mara ili kuepuka magonjwa ya milipuko.
Dauson, amesema Manispaa katika kuadhimisha siku hiyo ,imeona vyema kushirikiana na jamii kufanya usafi ikiwa ni njia moja wapo ya kuelimisha jamii kuhusiana na masuala ya usafi kwa kupenda mazingira yaliyo safi kwa usalama kwa afya zao.
Kwa upande wa Afisa afya Manispaa ya Morogoro,Ndimile Kilatu, amesema wapo watu ambao hawafanyi usafi mpaka kusimamiwa na kuonya kuwa wahakikishe wanatii sheria bila shuruti kwani suala la uchafuzi wa Mazingira halina msamaha.
“Uchafu unaozalishwa na mtu mmoja huathiri watu zaidi ya mia moja kwani huweza kusababisha mlipuko wa magonjwa, hatuhitaji kubembelezana katika suala la mazingira wanaochafua mazingira wachukuliwe hatua za kisheria tunataka kuwa Jiji , hatuwezi kuwa Jiji kama bado mji wetu ni mchafu kila mmoja awajibike kuhakikisha Morogoro Manispaa inakuwa safi ” Amesema Kilatu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa