WATENDAJI wa Mitaa Manispaa ya Morogoro wameagizwa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa viashiria vyote vilivyomo katika mkataba wa lishe ili kuleta mabadiliko katika kuboresha hali ya lishe kuanzia ngazi ya kaya hadi jamii nzima pamoja na kuweka utaratibu maalum wa kuadhimisha siku ya lishe kwa kila Mtaa.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Utumishi Manispaa ya Morogoro,Shabani Duru, katika kikao kazi na Maafisa Watendaji wa Mitaa juu ya kukumbushana viashiria vya mkataba wa lishe ngazi ya Mitaa ,katika ukumbi wa Mikutano wa Manispaa Ofisi Kuu Mei 29-2025.
Akizungumza na Watendaji hao wa Mitaa, Duru ameeleza kuwa viashiria vinavyotakiwa kutekelezwa ni pamoja na Watoto kupatiwa chakula mashuleni, wakina mama wajawazito kuhudhuria kliniki ipasavyo na kupatiwa madini joto, Watoto kupatiwa vitamin A, Watoto wenye utapiamlo mkali kupatiwa huduma vituoni na utoaji wa fedha ipasavyo kwa ajili ya afua za lishe.
“Watendaji wote hakikisheni mnasimamia vigezo vya upimaji na vipaumbele vya viashiria vya lishe, na muhakikishe kuwa mnapata taarifa za hali ya lishe kwa Watoto chini ya miaka mitano, kufanya ufuatiliaji wa Watoto walioacha matibabu ya utapiamlo kwa kushirikiana na watoa huduma za afya ngazi ya jamii.” Amesema Duru.
Duru, amewataka Watendaji kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili wazazi watambue umuhimu wa kuchangia chakula cha Watoto mashuleni ili kukuza kiwango chao cha lishe, kuongeza usikivu na kupunguza tatizo la utoro kwa wanafunzi.
Hata hivyo,amewataka watendaji kuhakikisha kazi hizo za kusimamia masuala ya afua za lishe wanaziingiza katika mfumo wa kuongeza ufanisi na uwajibikaji kwa watumishi wa Serikali PEPMIS.
Naye Mkuu wa Divisheni ya Afya,Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe Manispaa ya Morogoro,Dkt.Maneno Focus, amesema ni muhimu kwa Watendaji kuweka mkazo zaidi katika kusimamia utekelezaji wa Mkataba wa lishe katika maeneo yao ya utendaji ili kufikia malengo ya mkataba,kwani hili in agizo la serikali ambalo kila Kiongozi katika eneo lake la utawala anatakiwa kulisimamia.
Kwa upande wa Mratibu wa huduma za Lishe Manispaa ya Morogoro, Ester Kawishe, amesema suala la lishe ni mtambuka hivyo jamii kwa kushirikiana na wadau mbali mbali pamoja na Serikali kuhakikisha wanajenga Vizazi vyenye watoto wenye afya na lishe bora ili kuepuka udumavu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa