HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro imejipanga kutumia kiasi cha sh.Bil.75.4 kutoka vyanzo vyake mbalimbali ikiwemo mapato ya ndani na fedha kutoka kwa wahisani kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018-2019.
Hayo yalibainishwa na Mchumi wa Manispaa ya Morogoro Ndg Sadoth Kaijage kwenye kikao cha bajeti cha kamati ya ushauri ya Wilaya kilichofanyika mjini hapa.
Kaijage alisema kuwa kwa kipindi cha mwaka mwaka wa fedha 2018-2019 Halmashuari inakisia kupokea kiasi cha ruzuku na kukusanya mapato ya ndani ya kiasi cha Sh. Bil. 75.4 kutoka vyanzo vya Halmashauri,serikali kuu,matumizi ya kawaida ,wahisani na uchangiaji wa huduma za afya.
Aidha alisema kuwa katika bajeti hiyo Halmashauri imezingatia mpango wa maendeleo wa Taifa,kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali ,mpango wa lishe na dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2020 -2025 ili kuhakikisha bajeti hiyo inamletea tija mwananchi.
Awali Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro Ndg.Yahaya Nania akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro alisema kuwa rasimu ya mapendekeo ya bajeti ya mwaka 2018-2019 imezingatia sheria ya bajeti namba 11 ya mwaka 2015 pamoja na ilani ya Chama cha Mapinduzi.
‘’Pia bajeti hii imezingatia maelekezo mbalimbali kutoka Wizara ya fedha na nyinginezo’’alisema Nania.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro John Mgalula alisema kuwa tayari halmashauri imeweka mikakati mbalimbali ya ukusanyaji wa mapato katika kipindi hiki cha mwaka 2018 -2019 ili kuweza kuongeza mapato yake ya ndani.
Mgalula alitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kupitia upya mfumo wa usimamizi na ufuatiliaji wa mapato kwa kuboresha maeneo ambayo yana upungufu ,kuendelea kuwashirikisha wadau ,kutoa elimu kwa walipa kodi pamoja na kufanya kaguzi mbalimbali ili kubaini mianya inayovujisha mapato.
‘’Mkakati mingine ni pamoja na kubinafsisha baadhi ya vyanzo vya mapato kama vile ushuru wa mabango pamoja na utumiaji wa mfumo wa kielektroniki katika vyanzo vyote vya mapato ya ndani.’’alisema Mgalula.
Hata hivyo Mkurugenzi alisema Halmashauri imeweka kipaumbele katika ukusanyaji mapato,usafi wa mji ili kuweza kufikia lengo la kuwa jiji ,utawala bora ,afya ,maji ,ujenzi na uendelezaji wa viwanda.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa