MANISPAA ya Morogoro imefanya ziara yake ya kimafunzo ya usimamizi wa miradi miradi ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya huku wakifurahishwa na Jiji la Mbeya jinsi lilivyojipanga katika kuwaletea maendeleo wananchi wao.
Ziara hiyo ya kimafunzo iliyoanza Juni 19-2024 imehitimishwa Juni 21-2024 ambapo Madiwani wa Manispaa ya Morogoro wamesema yale mazuri yote ambayo wenzao wamekuwa wakiyafanya wataenda kuyafanyia kazi.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ziara hiyo, Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amesema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa sana ambapo wanaamini wakishirikiana kwa pamoja wataalamu na Madiwani yale ambayo yamefanywa na Jiji la Mbeya na wao wataweza kuyafanya na kufikia ile ndoto ya kuwa Jiji.
“Tumefika Jiji la Mbeya ,wenzetu wapo mbali sana , hata kwenye mapato wenzetu wana Bilioni 19 , lakini ndoto yetu ya kuwa Jiji inakaribia kwani hata hawa walivyokuwa Jiji hata mapato yao yalikuwa yanalingana na sisi japo sio sana , sisi mwaka unaoisha wa Bajeti 2024-2025 tunatarajia kufikia Bilioni 15 utaona ni kwa jinsi gani tunasogelea sifa ya kuwa Jiji”Amesema Kihanga.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato,Mhe. Kihanga, amesema kuwa wataongeza nguvu katika vyanzo vyote vya mapato ili waweze kutimiza malengo ya bajeti.
Upande wa vitega uchumi, Mhe. Kihanga anaamini kuwa vitega uchumi vilivyopo Manispaa ya Morogoro vikiongezewa umakini wa hali ya juu kuvitangaza na kukusanya vizuri mapato bado vitakuwa na msaada mkubwa wa kuongeza mapato kama wanavyofanya Jiji la Mbeya.
Aidha, ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Mbeya ilivyojipanga katika suala zima la usafi jambo ambalo limekuwa likisumbua Manispaa ya Morogoro.
“Wenzetu kwenye usafi wametuacha mbali sana , kuanzia uzoaji wa taka, ukusanyaji wa mapato, wenzetu wamejikita sana kulinda dampo la taka na kulisimamia lakini kuhusu ukusanyaji wa taka wameviachia vikundi kazi na makampuni jambo ambalo kwetu sisi tumebakia kusimamia dampo na ukusanyaji wa taka , kuna chakujifunza tutakaa na wataalamu wangu na madiwani tutaona na sisi namna ya kuboresha ili Mji wetu ambao ni Jiji tarajiwa liwe safi kama ilivyo kwa wenzetu wa Jiji la Mbeya” Ameongeza Mhe. Kihanga.
Maeneo ambayo ziara ili lenga ni ujifunzaji wa mfumo wa udhibiti wa taka ngumu, ukusanyaji wa mapato na ujenzi wa vitega uchumi.
Miongoni mwa maeneo ambayo yemetembelewa katika ziara hiyo ni Shule ya Msingi ya kulipia ya Azimio Pre & Primary inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, kitega uchumi cha City Park, Soko la Mwanjelwa, Shule ya Msingi Mkapa, Kiwanda cha usindikaji na mbogamboga kilichopo Iyela, Hospitali ya Igawilo Pamoja na Dampo la Nsalaga.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa