Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, ndugu Ally Machela amelaani vikali kitendo cha baadhi ya mgambo kuwapiga machinga, badala yake amewataka mgambo wajue kwamba kazi yao ni kusimamia usalama wa raia na sio kuwapiga ama kuwanyanyasa kwa namna iwayo yote ile na kwamba mgambo ye yote atakayebainika kwenda kinyume na maelekezo ya Manispaa katika kutekeleza majukumu yake, Manispaa itamchukulia hatua kali za kisheria.
Mkurugenzi Machela ameyasema hayo mapema asubuhi leo tarehe 21.11.2023 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa kituo cha redio na televisheni Abood, waliomtembelea ofisini kwake ili aueleze umma wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla mafanikio ambayo Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia Manispaa ya Morogoro imeweza kuyafikia ndani kipindi cha miaka miwili tangu mwaka 2021 hadi sasa.
“Hivi karibuni tulipokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya baadhi ya mgambo kumpiga mwanamke mmoja mjasiriamali na kumsababishia majeraha yaliyompelekea kulazwa hospitalini. Sisi kama Manispaa tunalaani kabisa kitendo hicho, na mgambo wote waliohusika kwenye tukio hilo tayari tumekwisha kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria na sisi kama Manispaa hatuwahitaji tena kwa ajili ya kufanya nao kazi” alieleza Machela.
Mkurugenzi Machela amewataka wafanyabiashara wote waendelee kuheshimu kufanya biashara kwenye maeneo waliyopangiwa na Manispaa huku wakifuata sheria zilizowekwa na Manispaa kuhusu ufanyaji wa biashara.
Vilevile, Mkurugenzi Machela amewataka machinga waliopo eneo la Faya wapuuze uvumi kwamba Manispaa itawafurusha kwenye eneo hilo mara baada ya ujenzi wa soko jipya la machinga kukamilika. Amesema kwamba Manispaa haina mpango wa kufanya hivyo na pia Manispaa haiwezi kuhamisha wafanyabiashara kwenye maeneo waliyopo sasa bila kushauriana na kushirikiana na viongozi wa Wilaya na Mkoa.
“Kwenye soko jipya la machinga linalojengwa kule Faya, tutawapeleka machinga waliopo mtaani, na zoezi la kuwatambua machinga hao tayari linaendelea kutekelezwa. Kwa machinga waliopo kwenye maeneo ya muda mfupi, wataendelea kuwepo na kufanya shughuli zao kwenye maeneo hayo. Kadiri tutakapokuwa tukijenga maeneo ya kudumu tutaendelea kuwahamisha” alifafanua Machela.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Machela ameueleza umma mafanikio ambayo Manispaa ya Morogoro imeweza kuyafikia katika sekta za elimu, afya, ardhi, biashara, Barabara, kilimo, mifugo na uvuvi kwa kipindi cha miaka miwili tangu mwaka 2021 hadi sasa, kupitia fedha kutoka Serikali Kuu na Makusanyo ya Mapato ya Ndani ya Manispaa.
“Katika sekta ya afya Manispaa tumefanikiwa kujenga Zahanati 12, vituo vya afya viwili, na hospitali moja ya Wilaya iliyopo kwenye Kata ya Mkundi. Sekta ya Elimu Msingi tumejenga shule mpya nne kwenye Kata za Mafisa, Mindu, Kihonda Maghorofani na Kilakala. Sekta ya Elimu Sekondari tumejenga vyumba vya madarasa 167 kwenye shule mbalimbali zilizokuwa na upungufu wa madarasa, tumejenga shule mpya nane kwenye Kata za Mbuyuni, Mazimbu, Tungi, Mkundi, Lukobe, Mindu, Mzinga na Boma, na shule sita kati ya hizo mpaka sasa zinao wanafunzi wa kidato cha kwanza na pili huku mbili zilizosalia ziko katika hatua ya ukamilishaji.
Pia, katika sekta ya ardhi tumefanikiwa kutatua migogoro 3,727 ya ‘double location’ kwa kupitia mradi wa Manispaa wa upangaji na upimaji wa ardhi kwenye eneo la Kiegea, hivyo kwa sasa Manispaa haina mgogoro wo wote wa ‘double location’ ya ardhi. Na kwa upande wa kilimo, wakulima zaidi ya elfu nane wananufaika na mbolea za ruzuku kutoka Serikali Kuu, tunaanzisha kilimo cha zao la karafuu na tunajenga machinjio mpya ya kisasa huko kwenye Kata ya Mkundi kwani machinjio tuliyo nayo sasa bado ni ile iliyojengwa miaka ya 1950, ambayo kwa sasa haikidhi mahitaji ya idadi ya wananchi waliopo sasa na inachangia kwa kiasi fulani uchafuzi wa mazingira” Alieleza kwa kina Machela.
Mkurugenzi Machela amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Manispaa kufikisha huduma za maendeleo kwa wananchi wake kupitia fedha nyingi za miradi ambazo Serikali imekuwa ikizileta kwenye Manispaa na kufanikisha utekelezaji wa miradi kwenye sekta za elimu, afya, kilimo na hata ardhi.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa