Murugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro , Sheilla Lukuba, amewakumbusha Wauguzi Manispaa ya Morogoro kutoa huduma kwa kuzingatia kanuni na taratibu kama walivyojifunza.
Hayo ameyasema leo Mei 12, 2020 Ofisini kwake, mara baada ya mahojiano na waandishi wa habari juu ya kuadhimisha Siku ya Uuguzi Duniani ambayo hufanyika Mei 12, kila mwaka.
Aidha, amewataka ,Wauguzi kuendelea kutekeleza majukumu ya kazi kwa kuzingatia kanuni na taratibu za kitaaluma kwa lengo la kutoa huduma bora za afya kwa wagonjwa.
Hata hivyo, amewakumbusha wauguzi kuzingatia mafunzo yanayotolewa mahala pa kazi kwani ndio yanayochochea kutoa huduma bora ya afya kwa wagonjwa.
Amewataka wauguzi kutambua kwamba huduma wanayotoa kwa wagonjwa ni huduma ya kibinadamu kwani elimu inachangia kufikia malengo ya kutoa huduma bora.
“Hivi sasa mambo yetu yanakwenda vizuri. Juzi juzi wakati wa Uzinduzi wa Wodi ya wazazi Regina Chonjo Sabasaba , tulipata ripoti nzuri ya kuhusu wakina mama wanao jifungua katika Vituo vyetu vya afya kupitia taarifa ya Kituo cha afya cha Sabasaba, ni jambo jema na mmeonyesha ni jinsi gani mlivyo makini katika utendaji wenu wa kazi, Malalamiko mengi yamepungua lakini ukifuatilia utabaini kwamba malalamiko mengi ni ya wagonjwa au mgonjwa kutaka kupewa kipaumbele kupata huduma ya afya badala ya kufuata utaratibu, tuwe makini na tufanye kazi hii kwa moyo mmoja na kama kuna changamoto ipo sehemu ya kusemea na kusikilizwa tunataka Manispaa yetu iwe mfano katika utoaji bora wa huduma na wananchi wafurahie na kuja kwetu badla aya kuhamia katika Hospitali binafsi ” amesema Lukuba..
Lukuba, amewapongeza wauguzi kwa kutekeleza majukumu ya kutoa huduma za afya kwa kuzingatia taratibu za kitaaluma kwa asilimia 100.
Katika hatua nyengine, amepinga vikali vitendo vya udhalilishaji kwa wauguzi huku akitaka vifanyiwe kazi kwa kuwa vitendo hivyo vinawapunguzia ari ya kufanya kazi.
“Sijawahi kupata malalamiko haya lakini kama vitendo hivi vipo katika Manispaa yetu iwe mwiko na ni marufuku , vikitokea na tukambaini aliyefanya vitendo hivi tutamchukulia hatua kali za kisheria, kwani lengo ni kuwahudumia wananchi wetu kwa ari kubwa sasa tukiwa na vitendo hivi vya udhalilishaji tunawapunguzia ari ya kufanya kazi Waauguzi wetu” Ameongeza Lukuba.
Amesema bado ipo haja ya kuendelea kuwapatia wauguzi mafunzo mbalimbali ambayo yatawasaidia zaidi kutoa huduma bora za afya kwa wagonjwa.
Naye, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro, Dr. Ikaji Rashidi, amewataka wauguzi kutoa taarifa kwa uongozi wa Manispaa endapo watadhalilishwa wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria.
“Mmesikia jamani nendeni mkawaeleze wenzenu kwamba endapo muuguzi atadhalilishwa, bila kuchelewa naomba atoe taarifa kwa uongozi ili wanaofanya hivyo tuwafikishe mbele ya vyombo vya dola,” amesema Dr. Ikaji..
Maadhimisho hayo hufanyika Mei 12, kila mwaka na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Wauguzi Sauti inayoongoza Afya kwa Wote.” Mwaka huu kitaifa maadhimisho yanafanyika mkoani Katavi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa