MKUU wa Wilaya ya Morogoro , Mhe. Regina Chonjo, amemuagiza Mkuu wa Shule ya Sekondari Mji Mpya, Mwalimu Zakayo John, kutotoa vyeti vya kuhitimu kidato cha nne kwa wanafunzi wote waliohusika na uharibifu wa mioundombinu katika shule hiyo.
Agizo hilo amelitoa leo Novemba 15, 2019, wakati akitembelea Shule hiyo ili kuona maeneo ambayo wanafunzi walifanya uharibifu.
Akizungumza na Waandishi wa habari, amesema Wanafunzi waliofika na Wazazi wao wataadhibiwa kwa viboko mbele ya wazazi wao na kupewa adhabu ndogo ndogo lakini wale waliokaidi wito hawatapa vyeti vya kuhitimu elimu yao ya kidato cha nne.
Aidha , amewataka wanafunzi wote kuacha uharibu wa miundombinu badala yake wafanye kile kilichowapeleka ili kukwepa adhabu na kuchukuliwa hatua za kinidhamu.
" Wanafunzi hamjambo? natumaini mmefurahia mazingira haya tofauti na yale mliyokuwa nayo, lakini ni kwanini mnashindwa kuyatunza? mmeanza kuharibu miundombinu ya shule na kuiba taa za shule, Serikali imejenga Shule hii ili msome na mpate elimu bora kwa maendeleo yenu, sasa hawa wenzenu walikosa aibu na nidhamu kwa uharibifu huu nataka waadhibiwe na viboko mbele ya wazazi wao na kupewa adhabu za kupanda miti , wale wa kidato cha nne waliohusika nawapa siku saba kuanzia leo waripoti shuleni wamwagilie miti wasipofanya hivyo nawao tunawafungia matokeo yao na kuwanyima vyeti na wale wa kidato cha tatu wakati wa likizo asubuhi mfike na muhakikishe miti yote ina mwagiliwa na asikose mtu" Amesema DC Chonjo.
Amesema Shule hiyo haijafunguliwa rasmi na imejengwa kwa thamani kubwa ya fedha takribani Bilioni 1 na Milioni 400 zimetumika katika ujenzi huo , hivyo katika kuwasaidia wanafunzi wasome waliona ni vyema wakamuomba Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Selemani Jaffo, ili kuitumia lakini cha kushangaza wanafunzi wapuuzi wameanza kuonesha tabia chafu.
"'Nipende kuwaeleza Wanafunzi sisi tunawapenda sana, tumeamua Shule hii iwe miongoni mwa shule zitakazo toa masomo ya ngazi ya juu ya elimu ya Sekondari A. Level, lakini mmeanza kuharibu miundombinu je tutafika kweli? nilitarajia siku moja mnipatie ugeni rasmi katika Mahafali yenu lakini kwa hatua hii kwakweli mnanitia mashaka, sasa nafasi mliyonayo muitumie vizuri, kwani uchumi wa Viwanda unategemea Taifa lenye Elimu"" Amesisitizia DC Chonjo.
Amesema hakutakuwa na Viwanda kama hakuna wataalamu wenye uelewa wa kutosha wa kuendesha Viwanda, hivyo amewataka Wanafunzi wajirekebishe na kujenga tabia njema kwani hategemei kurudi katika Shule hiyo kwa kosa hilo.
Naye, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, amewaomba Wanafunzi wabadilike na kuachana na tabia mbaya ya kuharibu miundombinu ya Shule.Amewataka Wanafunzi wanapokwenda Shule , wawe na wazo moja la kusoma na si vinginevyo.
Katika hatua nyengine, Mstahiki Meya , Mhe. Pascal Kihanga, amemuomba Mkurugenzi wa Manispaa ya Halmashauri ya Morogoro, kuwapatia Shule hiyo jumla ya miche 300 ya miti kwa ajili ya kuboresha mazingira katika Shule hiyo.
"' Mkurugenzi nikuombe pale Manispaa tuna bustani ya miche, wapatie Shule hii miche 300 kwa kuanzia na jua kuna Wanafunzi ambao vichwa vyao ni vibaya watang'oa, , kwakuwa wamesema hawana bajeti ya kununua miche, tuanze na hiyo ili tuipendezeshe shule hii kwani mazingira yaliyopo kwa sasa hayaendani na ubora wa shule ilivyo" Amesema Mhe. Kihanga
Katika kuona miti hiyo inastawi, amemtaka Mkuu wa Shule kuhakikisha mara baada ya kupokea miche hiyo, wahakikishe kila mwanafunzi anapatiwa mti wake kwa ajili ya kuumwagilia asubuhi na jioni kabla ya kurudi nyumbani.
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Mji Mpya, Mhe. Wenseslaus Kalogeries, amewataka Wanafunzi hao kulinda miundombinu ya shule na kila mmoja awe mwangalizi wa mwenzake na endapo kuna mwanafunzi amefanya uharibu atoe taarifa kwa mwalimu.
Amesema watakutana na Bodi ya Shule ili kuhakikisha matukio kama hayo hayatokei tena katika Shule hiyo na kumtaka Mkuu wa Shule kuwasilisha taarifa za wanafunzi watukutu wote kwenye bodi ya shule ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa