MKUU wa Mkoa wa Morogoro , Mhe. Adam Malima, ameipongeza Manispaa ya Morogoro kwa kupata hati safi kwa kipindi cha miaka nane (8) mfululizo kwenye ukaguzi wa fedha mwaka 2021/2022.
Pongezi hizo amezitoa katika Kikao Maalum cha Baraza la Madiwani la kujadili utekelezaji wa hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka wa fedha 2021/2022 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa juni 22/2023.
Akizungumza katika Mkutano huo, RC Malima, ameitaka Manispaa ya Morogoro kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa na mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za Serikali CAG ili kuendelea kupata hati safi.
"Ninampongeza Mkurugenzi na watendaji wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana vyema na Baraza la Madiwani kwa utendaji kazi mzuri ulioleta matokeo mazuri na kuiwezesha Halmashauri kupata hati safi kwa kipindi cha miaka nane , lakini niwaombe Madiwani hii Manispaa ni yenu watendaji hawa ni wapita njia tu, tushikamane kuhakikisha tunaboresha huduma za jamii kama Ilani ya CCM inavyotaka chini ya Mwenyekiti wake ambaye ndiye Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan .”Amesema RC Malima.
Vilevile ameitaka Manispaa kusimamia vyanzo vya mapato vilivyopo ndani katika kuongeza mapato ya Halmashauri na sio kutegemea vyanzo vya nje.
Akisoma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Mkoa wa Morogoro, CPA, Peter Mwabwanga, amesema Manispaa ya Ubungo ilikuwa na hoja 68 ambapo kati hizo hoja 58 zilijibiwa vizuri na hoja 10 zimebakia na hoja 6 mpya na hoja 4 za zamani.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma, amewataka watendaji na watumishi kuhakikisha kwamba wanawapatia ushirikiano mzuri Madiwani wanapotaka kuongea na wananchi wao katika kutatua kero na changamoto za wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Rebeca Nsemwa, ameipongeza Manispaakwa kupata hati safi, hati hiyo imekuja kutokana na ushirikiano baina ya Baraza la Madiwani, Mkurugenzi, Wataalamu , Chama Cha Mapinduzi CCM pamoja Pamoja na watumishi kwa kufanya kazi kwa kujituma na kufuata vigezo na malengo waliyojiwekea.
Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Mazimbu , Mhe. Pascal Kihanga, amewataka watendaji kujitahidi kukusanya mapato pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kuweza kushughulikia changamoto za Wananchi.
Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro amesema kuwa haya ni mafanikio makubwa sana kwa Manispaa , kwani kitendo cha kupata hati ya ukaguzi inayoridhisha kwa muda wa miaka nane mfululizo imetokana na utendaji kazi mzuri unaooneshwa na watumishi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa