MKUU wa Mkoa wa Morogoro , Mhe. Martine Shigela, ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kupata hati safi kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo kutoka mwaka 2015/2016 mpaka mwaka 2019/2020.
Pongezi hizo zimetolewa Juni 16/2021 katika kikao maalum cha Baraza la madiwani cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2019/2020, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano Soko Kuu la Chifu Kingalu Morogoro.
Sambamba na pongezi hizo, RC Shigela, amewasifu watendaji wa Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani kwa utendaji wao mzuri wa kazi na kujituma kwa kuwahudumia wananchi wa Manispaa ya Morogoro.
"Ninampongeza Mkurugenzi na watendaji wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana vyema na Baraza la Madiwani kwa utendaji kazi mzuri ulioleta matokeo mazuri na kuiwezesha Halmashauri kupata hati safi kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.”
Aidha, RC shigela, ametoa rai kwa watumishi wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kutumia utaalamu wao katika utendaji kazi wao na pia kufanya kazi kama timu moja katika kuwahudumia wananchi.
Vilevile amewataka kusimamia vyanzo vya mapato vilivyopo ndani katika kuongeza mapato ya Halmashauri na sio kutegemea vyanzo vya nje.
Aidha ametoa wito kwa wakuu wa Idara kutoa mafunzo ya kazi kwa vitendo(On job Training) ya mara kwa mara kwa watendaji wao ili kuhakikisha kazi zinafanywa vizuri na kwa ufanisi.
Katika hatua nyingine, RC Shigela, amewataka watendaji wasiopeleka fedha benki wapeleke kwa wakati na wasiofanya hivyo waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Hata hivyo ,ameagiza kufungwa kwa mfumo wa uhakika wa mapato kwenye Stendi ya mabasi ya Msamvu pamoja na kusimamia vyanzo vikubwa vya mapato ambapo hadi kufikia Agosti mwaka 2021 mfumo huo uwe umeshakamilika.
Pia amezitaka Taasisi za Serikali kuacha tabia ya kupelekana Mahakamani jambo ambalo amelipinga vikali huku akizitaka Taasisi hizo ambazo zinakesi wahakikishe ndani ya wiki moja wamefuta kesi hizo na kufanya majadiliano yao nje ya mahakama.
Hata hivyo,amesema yupo katika hatua ya kukutana na wakazi wanaoishi katika eneo la Star City kabla ya kukutana na mmiliki wa eneo hilo ili kuweza kujadiliana nao na kuona jinsi ya kuweza kuondoa changamoto zinazowakabili .
Aidha, amewataka watendaji na watumishi kuhakikisha kwamba wanapatia ushirikiano mzuri Madiwani wapotaka kuongea na wananchi wao katika kutatua kero na changamoto za wananchi.
Mwisho RC Shigela, ameutaka Uongozi wa Manispaa ya Morogoro kuhakikisha kwamba wanayashughulikia magari yote ambayo ni mabovu kwa kuyafanyia matengenezo ili yaweze kufanya kazi pamoja na kupitia mkataba wa Kampuni ya usafi wa Kajenjere ili kuona namna gani ya kuweza kutatua changamoto ambazo wananchi wamekuwa wakizielekeza kwao.
Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro na Diwani wa Kata ya Mazimbu , Mhe. Pascal Kihanga, amewataka watendaji kujitahidi kukusanya mapato pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kuweza kushughulikia changamoto za wafanyabiashara wa Soko Kuu la Chifu Kingalu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa