Wilaya ya Morogoro imeadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kupanda miti, kufanya usafi wa mazingira, na kufanya mashindano ya uandishi wa insha kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Mengine ni bonanza la michezo, mahojiano na wazee kuhusu masuala ya muungano na kuwa na mkesha wa pamoja uliojumuisha kutazama na kusikiliza hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyorushwa moja kwa moja kutokea Ikulu, usiku wa tarehe 25.04.2024.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 26.04.2024 na Katibu Tawala Msaidizi wa Wilaya ya Morogoro, ndugu Hilary Sagala, alipokuwa akizungumza na wananchi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, katika kilele cha maadhimisho ya Siku Kuu ya Muungano, kilichofanyika kwenye eneo la stendi ya zamani ya daladala Manispaa ya Morogoro.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mheshimiwa Pascal Kihanga, amesema kwa tulipofika sasa, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hauwezi kuvunjika kwani viongozi wa pande zote mbili wamekuwa wakiendelea kuhakikisha masuala ya muungano yanashughulikiwa ipasavyo kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Morogoro ndugu Emmanuel Mkongo, amewashukuru watu wote waliojitokeza kushiriki kwenye maadhimisho hayo na amewataka wananchi waendelee kuuenzi na kuulinda muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuwa ni miongoni mwa tunu za Taifa la Tanzania.
Wilaya ya Morogoro inaundwa na Halmashauri ya Wilaya Morogoro na Halmashauri ya Manispaa Morogoro.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa