Afisa Utumishi Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Waziri Kombo , amekutana na Watendaji wa Kata zote 29 pamoja na Watendaji wa Mitaa, Maafisa Afya kwa ajili ya kuwasilisha taarifa za jinsi gani walivyochukua hatua katika maeneo yao dhidi ya kujikinga na ugonjwa wa CORONA.
Mkutano huo wa kuwasilisha taarifa na kujadiliana juu ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA umefanyikika leo Machi 26 , 2020 katika Ukumbi wa Mikutano wa Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, amesema lengo la mkutano huo ni kufanya tathimini juu ya hatua zilizochukuliwa na Maafisa Afya wa Kata pamoja na Watendaji dhidi ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Amesema tangia Serikali itangaze taratibu za Kujikinga , kwa upande wa Manispaa hali ya utoaji wa elimu imefanyika kwa kiasi kikubwa sana na mapokeo ni mazuri licha ya kuwepo kwa maeneo machache ambayo yamekuwa chini sana katika mapokeo ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.
Aidha, amewataka Maafisa Afya pamoja na Watendaji kushirikiana kikamilifu na kuunda timu ndogo ambayo ikatakuwa inafanya ufuatiliaji kuanzia ngazi zote na maeneeo yote ambayo yana mkusanyiko, kwenye maduka, Hoteli, Nyumba za Ibada pamoja na Stendi za Mabasi ili kuoana hali ya utekelezaji ikoje katika maeneo hayo.
“Kiujumla katika Manispaa yetu ya Morogoro tumejitahidi sana kuelimisha Wananchi , tumekuwa tukitumia njia mbalimbali kama vile matangazo ya vipeperushe, Magari mitaani, Vyombo vya habari, lakini sasa tumekwenda mbali zaidi kwa kugawana majukumu na kuunda timu tatu ambazo zitakuwa zikifanya kazi za ufuatiliaji ikiwemo timu itakayopitia Hotelini, Vitu vya Mabasi na Bodaboda na ile itakayopitia katika Maduka ya Dawa na kawaida ili kuona kama Vitakasa mikono vinazingatia bei elekezi ya Serikali” Amesema Kombo.
Hata hivyo ametoa agizo kwa Maafisa Afya wote na Watendaji katika ngazi za Kata na Mitaa kuhakikisha kila mwezi wanatoa taarifa jinsi gani wameshughulikia suala hilo kikamilifu katika maeneo yao na taarifa hizo ziwasilishwe kwa Afisa Afya wa Manispaa ambaye atatoa fomu maalumu za kujaza.
Naye Kaimu Afisa Afya Mkoa, Prisca Gallet, ameipongeza timu ya Waatalamu pamoja na Maafisa Afya wa Kata na Watendaji kwa jitihada walizochukua za kutoa elimu ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA licha ya kuwepo na changamoto za baadhi ya maeneo kutofuata taratibu hizo.
Amesema mipango iliyopo ni kuhakikisha maeneo yote yaliyopo Manispaa ya Morogoro yanatenga Maji tiririkia na sabuni pamoja na Vitakasa Mikono na kwa wale watakao kaidi watachukuliwa hatua kali za kisheria.
‘Tumeanza kuona matokeo mazuri, hata katika pita pita yangu nimeona tunajitahidi hongereni sana wataalamu , lakini tusibweteke Ugonjwa huu kama mnavyojua ni mgeni katika Nchi yetu , sasa tuanakila sababu za kufuata maelekezo ya Viongozi wetu wa Ngazi za Juu pamoja na Wataalamu wetu wa Afya, tukifanya hivyo na kila mtu akifanya kwa nafasi yake tutakuwa salama katika kujikinga na Ugonjwa huu, kikubwa Maafisa Afya na Watendaji mshirikiane kikamilifu na kila Kata ichukue tahadhari kubwa ya kuwaelimisha Wananchi wake”Amesema Gallet.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa