SURA NA TASWIRA YA HALMASHAURI YA MANISPAA YA MOROGORO
Utangulizi
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ni mojawapo ya Halmashauri 6 za Mkoa wa Morogoro, ambazo ni Mvomero, Manispaa Morogoro, Kilosa, Kilombero na Ulanga. Aidha ni Halmashauri hii ndio Makao Makuu ya Mkoa wa Morogoro.
Wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ni mchanganyiko wa makabila mbalimbali. Kabila ambalo ni wenyeji wa Halmashauri hii ni Waluguru. Morogoro ilipanda kufikia hadhi ya kuwa mji mwaka 1962. Kasi ya kupanuka kwa Halmashauri ya mji iliongezeka kidogo kidogo na ilipofika tarehe 1/7/1988 ikapanda hadhi na kuwa Manispaa. Kutokana na fursa mbalimbali zilizopo kijiografia, kiuchumi na kimazingira, jitihada zinafanyika kupitia Halmashauri na Wadau mbalimbali kuendeleza Manispaa katika nyanja mbalimbali ili kufikia hadhi ya Jiji siku za usoni.
1.1 Mahali:
Manispaa ya Morogoro iko umbali wa Kilometa 195 kutoka Jiji la Dar es Salaam. Ipo kati ya Latitudo 4.5 Kusini na Longitudo 37.4 Mashariki. Ipo kiasi cha futi 1,600 kutoka usawa wa bahari.Manispaa inapakana na milima ya Uluguru kwa upande wa Kusini na Milima ya Mindu kwa upande wa Magharibi. Upande wa Kaskazini inapakana na Wilaya ya Mvomero na Morogoro kwa upande wa Mashariki.
1.2 Eneo:
Halmashauri ya Manispaa ina eneo la Kilometa za Mraba 531.04 sawa na asilimia 0.8 ya Mkoa wa Morogoro wenye eneo la Kilometa za mraba 72,939.
1.3 Hali ya Hewa
Wastani wa joto ni nyuzi 100C hadi 140C wakati wa baridi (Juni – Agosti) na wakati wa joto (Novemba – Desemba) kati ya nyuzi 280C hadi 300C. Ipo misimu miwili ya mvua: Mvua za vuli na Mvua za Masika. Mvua hizo hunyesha kwa wastani wa kati ya milimita 821 hadi 1,505.
1.4 Idadi ya Watu
Manispaa ya Morogoro imekuwa ikipanuka kwa kasi kutokana na ongezeko la watu. Kwa mujibu wa takwimu ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2002, idadi ya watu imeongezeka kutoka 24,999 mwaka 1967 hadi watu 227,921 mwaka 2002. Wastani wa ongezeko la watu kwa mwaka ni asilimia 4.7. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro inawakazi wapatao 315,866 wakiwemo wanaume 151,700 na Wanawake 164,166.
Sababu inayochangia kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu ni pamoja na: Kuzaliana na kuhamia. Sababu zinazochangia kasi kubwa ya kuhamia ni pamoja na :
1) Ongezeko la viwanda vidogo na vya kati
Ongezeko la sehemu za biashara
Ongezeko la shughuli za kilimo na ufugaji
Uboreshaji wa miundombinu
Kupanuka kwa huduma za kijamii – mfano: shule, vituo vya afya, sehemu za starehe.
1.5 Shughuli za Kiuchumi na Ajira
Shughuli kuu zinazofanywa na wakazi wa Manispaa ni pamoja na:
Biashara – Jumla na reja reja
Kilimo na Mifugo –
Shughuli za ofisini
Ajira ndogo ndogo
Viwanda
Kilimo cha Mazao yanayolimwa nje kidogo ya Mji na katika Wilaya jirani za Mvomero na Morogoro ni pamoja na, mpunga, mahindi, mkonge, ndizi, mihogo, Matunda na mboga za majani.
1.6 Muundo wa Utawala:
Halmashauri ya Manispaa ina Tarafa moja (1) yenye Kata 29 na Mitaa 272. Ongezeko la Kata kutoka 19 hadi kufikia 29 inatokana na ongezeko la Watu ambapo baadhi ya Kata za Zamani zimegawanywa. Kata zilizoongezwa ni Luhungo, Kauzeni, Magadu, Lukobe, Mkundi, Chamwino, Kihonda Magorofani, Mindu, Mafisa na Tungi.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambalo ni chombo cha juu cha kutolea maamuzi lina jumla ya Madiwani 42. Kati yao Madiwani 29 ni wa kuchaguliwa kutoka kata 29 za Halmashauri na miongoni mwao 24 ni wanaume na watano (5) ni wanawake. Aidha, Madiwani kumi 10 ni wa kuteuliwa kutoka Chama tawala cha CCM. Madiwani 3 (watatu) waliosalia ni Wabunge, mmoja anawakilisha Jimbo la Morogoro Mjini na 2 ni wa Viti maalum.
Katika mfumo wa Utendaji, Manispaa ya Morogoro ina Idara kumi na tatu na Vitengo sita vinavyowajibika moja kwa moja kwa Mkurugenzi. Idara kumi na tatu za Halmashauri ni:
Utawala na Utumishi
Fedha na Uongozi
Afya
Elimu Msingi
Elimu Sekondari
6) Mipangomiji na Ardhi
7) Maji
8) Maendeleo na Ustawi wa Jamii
9) Mifugo na Uvuvi
10)Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika
11)Mipango,Takwimu na Ufuatiliaji
12)Usafi na Mazingira
13)Ujenzi na Zimamoto
Vitengo vitano ni:-
1) Sheria
2) Ukaguzi wa Ndani
3) Ugavi
4) Uchaguzi
5) Ufugaji Nyuki
6) Teknologia,Habari, Mawasiliano na Uhusiano
Manispaa kama chombo cha utawala, kinatawala kwa mtindo wa Kamati. Kuna Kamati kuu tano ambazo ni
i) Kamati ya Fedha na Uongozi
ii) Kamati ya Huduma za Uchumi, Elimu na Afya
iii) Kamati ya Mipangomiji na Mazingira
iv) Kamati ya kudhibiti Ukimwi
v) Kamati ya Maadili.
1.7 Idadi ya Watumishi:
Kwa Mwaka 2010/2011, Halmashauri ina jumla ya watumishi 3123 wa kada mbalimbali.Idara ya Elimu (Msingi na Sekondari) ina watumishi 2425 sawa na asilimia 77.6 ya watumishi wote.
2.0 Maendeleo ya Kisekta
Sekta zote za Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro zinatekeleza majukumu yake ya msingi kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2011 - 2015, Dira ya Maendeleo ya 2025, Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA) II na Malengo ya Millenia ili kutoa huduma bora kwa jamii. Maelezo ya kila sekta yameainishwa kama ifuatavyo.
2.1 SEKTA YA ELIMU
Utangulizi:
Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025 inalenga katika kutokomeza kabisa umaskini ifikapo mwaka 2025, na hivyo kipaumbele kikubwa kimewekwa katika Sekta ya Elimu ambayo inachukuliwa kama msingi mkubwa katika kuleta mabadiliko kijamii na kiuchumi. Hivyo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro haiko nyuma katika kudumisha mikataba na makubaliano ya Kimataifa yanayohusu upatikanaji, usawa na ubora wa Elimu.
2.1.1 Taasisi za Elimu:
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ina Taasisi 218 zinazotoa Elimu kwa ngazi mbalimbali. Ikiwa ni pamoja na Elimu ya Awali, Elimu ya Msingi, Elimu ya Sekondari, Elimu ya Ualimu, Elimu ya Ufundi na Elimu ya Juu. Aidha jumla ya Taasisi 72 zinamilikiwa na watu binafsi na madhehebu ya dini na Taasisi 146 zinamilikiwa na Halmashauri/Serikali. Orodha na idadi ya taasisi hizo imeonyeshwa katika jedwali Na.2
Jedwali Na 2 - Idadi ya Taasisi zilizopo Manispaa ya Morogoro:
MAELEZO
|
TAASISI ZA SERIKALI |
TAASISI ZA BINAFSI |
JUMLA |
Shule za Awali
|
56 |
23 |
79 |
Shule za Msingi
|
62 |
23 |
85 |
Shule za Sekondari
|
23 |
25 |
48 |
Vyuo vya Ualimu
|
1 |
- |
1 |
Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi
|
1 |
- |
1 |
VETA
|
1 |
- |
1 |
Vyuo vikuu
|
2 |
1 |
3 |
JUMLA KUU
|
146 |
72 |
218 |
Chanzo: Ofisi ya Elimu 2014
2.1.2 Elimu ya Msingi:
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ina jumla ya shule 85 za Msingi, kati ya hizo shule 62 ni za Serikali na shule 25 zisizo za Serikali. Jumla ya wanafunzi walio katika shule za msingi za Serikali ni 50,448 kati yao wavulana ni 24,891 na wasichana ni 25,557.
2.1.3 Mpango wa Elimu ya Msingi kwa walioikosa (MEMKWA)
Mpango huu unasimamia watoto wanaostahili kwenda shule na hawakupata fursa .Watoto hawa wanaandikishwa katika shule ya Msingi.MEMKWA ina jumla ya Wanafunzi 251, kati yao Wavulana ni 146 na wasichana ni 105.
2.1.4 MUKEJA
Huu ni mpango kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii,kundi hili lina jumla ya Washiriki 233.Katika mpango huu wanakisomo hupata mbinu za kujiajiri kama ushonaji,Useketaji,Ususi,Ufinyanzi,Ufumaji,Ufugaji,Kilimo na bustani,ufundi cherehani na utunzaji wa Mazingira.Pia kuna wanakisomo chenye manufaa KCM Washiriki 157,Wanakisomo cha kujiendeleza washiriki 76.
2.1.5 Vituo vya Ufundi Stadi:
Manispaa ina vituo viwili (2) vya Ufundi Stadi vyenye wanafunzi 131, wakiwemo wasichana 79 na wavulana 52 waliomaliza Elimu ya Msingi na ambao hawakupata nafasi ya kujiunga na Elimu ya Sekondari. Vituo hivi ni Msamvu na Luhungo ambavyo hufundisha Useremala na Sayansi Kimu. Wanafunzi hawa baada ya kumaliza mafunzo haya hujiajiri au kuajiriwa katika fani walizosomea.
3.0 Elimu ya Sekondari:
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ina shule 48 za sekondari, kati ya hizo shule 23 ni za Serikali na 25 zinamilikiwa na watu binafsi na taasisi za dini. Ongezeko la shule za sekondari na madarasa huchangia ongezeko la idadi ya watahiniwa wanaochaguliwa kujiunga na Elimu ya Sekondari.
4.0 Afya
4.1Utangulizi:
Idara ya Afya ina Vitengo Vikuu 3 ambavyo ni:
Kitengo cha Tiba
Kitengo cha Kinga na
Kitengo cha Usafishaji
Vituo vya Tiba:
Manispaa Ina jumla ya Vituo 60 vya Tiba ikiwa ni vya Serikali Kuu, Halmashauri, Mashirika ya umma na Watu binafsi kama ifuatavyo katika Jedwali Na 3.
Jedwali Na.3 – Aina na Idadi ya vituo vya Tiba katika Manispaa:
AINA YA KITUO |
SERI KALI KUU |
HALMA SHAURI |
HUDUMA BINAFSI BILA FAIDA |
MASHIRIKA YA UMMA |
HUDUMA BINAFSI KWA FAIDA |
JUMLA |
Hospitali
|
2 |
0 |
0 |
1 |
0 |
3 |
Vituo vya Afya
|
0 |
4 |
3 |
1 |
5 |
13 |
Zahanati
|
0 |
16 |
10 |
10 |
8 |
44 |
Jumla kuu
|
2 |
20 |
13 |
12 |
13 |
60 |
Chanzo: Ofisi ya Mganga Mkuu wa Manispaa 2014
5.0 Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji
5.1 Kilimo:
Shughuli za Kilimo kwa sehemu kubwa hufanyika kwenye Kata za pembezoni za Mbuyuni, Kihonda, Mzinga, Mazimbu, Kingolwira na Bigwa na pia katika baadhi ya maeneo ya wilaya za jirani za Morogoro vijijini na Mvomero. Mazao yanayolimwa ni pamoja na mahindi, mpunga, migomba, katani, mifugo. Mboga za majani na matunda yanalimwa pia.
5.2 Ushirika
Kitengo hiki kinashughulika na shughuli za uhamasishaji wa uanzishwaji wa vyama vya akiba na Mikopo. Manispaa ya Morogoro ina vyama vya aina mbalimbali vilivyoandikishwa. Pia kitengo hiki kinashughulika na ufuatiliaji na usimamizi wa sheria na kanuni zinazoongoza vyama vya ushirika, kuhakikisha kuwa mahesabu ya vyama hivyo yanakaguliwa kwa wakati unaotakiwa.
6.0 Mifugo:
Kuna shughuli mbalimbali za mifugo zinazofanyika mojawapo ikiwa ni kutoa elimu na ushauri wa mbinu bora za ufugaji kutoa huduma za matibabu na kinga ya mifugo, pia huduma mbalimbali kama kuhasi, uogeshaji na kupima mimba.
7.0 Mipangomiji na Ardhi
Katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2013 Halmashauri ya Manispaa Morogoro iliandaa michoro ya mipango miji ipatayo 57. Aidha jumla ya viwanja 4706 vimepimwa katika maeneo ya Kiegea A , Lukobe , Lukobe Q, Mkundi P, Mguru wa Ndege Q , Lukobe Kambi tano,Legeza Mwendo, Goronya, Kihonda N, na Tuelewane U.
7.1 Utoaji wa hati miliki:
Katika maeneo yaliyopimwa kuanzia mwaka 2010 hadi 2013 jumla ya hati zipatazo 3007 zimeandaliwa.
7.2 Urasimishaji wa makazi:
Katika Manispaa ya Morogoro urasimishaji umefanyika katika maeneo yafuatayo Kihonda B, Tuelewane, Falkland, Bigwa Kisiwani na Bigwa Sokoni.
7.3 Sekta ya Uhifadhi wa Mazingira:
Katika mwaka 2009/2010 hadi 2012/2013 sekta ya uhifadhi wa mazingira ilifanikisha upandaji wa miti 1,025,000 katika maeneo mbalimbali kama lengo la upandaji wa miti lilivyo kiwilaya ukilinganisha na Miti 1,799,300 iliyokuwa imeandaliwa kwenye vitalu mbalimbali.
8.0 Ujenzi na Zimamoto
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ina mtandao wa barabara zenye urefu wa km 632.03.Kati ya hizo km 50 zinahudumiwa na wakala wa Barabara Tanzania(TANROADS) na km 582.03 zinahudumiwa na Manispaa kama inavyoonekana hapo chini:-
Barabara za lami.........................................27.77
Barabara za changarawe.............................. 36.40
Barabara za vumbi/udongo........................... 524.86
9.0 Maji:
Maji ni rasilimali muhimu sana kwa maisha ya binadamu. Chanzo kikuu cha maji ni chemchem zitokazo milima ya Uluguru. Bwawa la Mindu ndilo tegemeo kubwa kama chanzo na ni hifadhi ya maji. Pampu ya maji iliyopo ina uwezo wa kusambaza maji katika eneo lenye ukuwa wa kilomita za mraba 1,014 tu. Jumla ya watu 24,500 ambayo ni sawa na 74.7% wanapata maji safi. Asilimia 23.3 iliyobaki, inatumia maji yasiyo safi kutoka visimani na katika mito. Mahitaji halisi ya maji kwa sasa ni kiasi cha mita za ujazo 39,440 kwa siku na huwa yanasambazwa na Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka (MORUWASA).
10. SEKTA YA MAENDELEO NA USTAWI WA JAMII.
Kazi kubwa ni kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusiana na maendeleo ya sekta mbalimbali za kiuchumi. Pia kubainisha matatizo yanayojitokeza kwenye jamii na jinsi ya kuyatafutia ufumbuzi wake kwa kufuata vipaumbele vya jamii husika. Katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo, hulenga kutatua matatizo yaliyojitokeza kwa kuzingatia sera, kanuni na sheria za nchi ikilenga kuwajengea watu kufanya maamuzi yao wenyewe na kujihusisha kwenye maendeleo yao wenyewe kwa ngazi zote mfano: Sera ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sera ya UKIMWI na Sera ya MKUKUTA.
Idara hii imegawanyika katika vitengo viwili:
i) Kitengo cha Maendeleo ya Jamii ambacho hulenga masuala ya maendekeo, jinsia na takwimu, UKIMWI na Mpango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (TASAF)
ii) Kitengo cha Ustawi wa Jamii huusisha watu hasa wenye ulemavu na wasiojiweza:
Wazee
Ombaomba
Watoto waishio katika mazingira hatarishi
Watu wenye mtindio wa ubongo, n.k.
Katika Manispaa ya Morogoro, vipo vituo mbalimbali vinavyojihusisha na utunzaji na malezi ya watoto waishio katika mazingira hatarishi, mtindio wa ubongo.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa