MANISPAA ya Morogoro imeendesha Mafunzo ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili kwa waandishi wasaidizi na waendesha vifaa vya kibayometriki (BVR) katika ukumbi wa Glonessy Nanenane Kata ya Tungi Mei 14-2025.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo, Afisa Mwandikishaji Jimbo la Morogoro Mjini, Faraja Maduhu ,amewataka wanasemina hao kuzingatia mafunzo hayo na kwenda kufanya kazi kwa ujuzi, uwezo na weledi walionao ili kutekeleza zoezi la Kitaifa la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili.
Maduhu, amewataka Waandikishaji hao wasihodhi zoezi hilo, kwani kama watakutana na changomoto yoyote wafanye mawasiliano na wataalam wa kutoka Kata, Jimbo au Taifa ili kuhakikisha zoezi hilo linatekelezwa kwa ufasaha.
Aidha, amesema uboreshaji huo utahusisha kuhamisha taarifa za wapiga kura waliohama kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo.
Naye Mjumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi, Balozi Omar Ramadhani Mapuri, amesema kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 11(1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume pia ina jukumu la kuandaa Daftari la Awali la Wapiga Kura na kuliweka wazi kwa umma.
Balozi, Mapuri, amesema lengo la uwekaji wazi wa Daftari hilo ni kutoa fursa kwa wananchi kukagua, kufanya marekebisho ya taarifa za wapiga kura na uwekaji wa pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa.
Mwisho,Balozi Mapuri, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia yale yote wanayofundishwa,kwa kuwa wasikivu na kufuata sheria,kanuni za Uchaguzi.
Aidha amewalekeza wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata kuwasiliana na watumishi wa tume huru ya Uchaguzi endapo watakutana na changamoto yoyote wakati wa utekelezaji wa uboreshaji wa daftari la kudumu la Mpiga kura.
Zoezi hilo la uandikishaji linatarajia kuanza Mei 16-22 mwaka 2025 ambapo vituo vitakuwa wazi kuanzia saa 2:00 Asubuhi hadi saa 12:OO jioni.
Kauli Mbiu ya Uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura 2025 "Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura, ni Msingi wa Uchaguzi Bora ".
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa