JUMUIYA ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT), imeipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa usimamizi mzuri wa Soko kuu la kisasa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Novemba 19,2019, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), Ndg. Stephen Mhapa, amesema kasi ya mradi huo imewafurahisha hivyo ameitaka Manispaa kuhakikisha sehemu iliyobakia ya ujenzi inakamilika kwa wakati uliopangwa.
Amesema kuwa, Manispaa ya Morogoro inahitaji kupongezwa sana kwani kabla ya pesa za ruzuku ya Serikali katika Miradi Mikakati tayari Halmashauri ya Manispaa ilishaanza kutafuta pesa kwaajili ya ujenzi , hizi ni juhudi kubwa sana , hatua iliyofikia ya mradi imeonesha thamani ya pesa iliyotumika.
Amemshauri Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa kuhakikisha inaweka vipaumbele vya miradi katika vikao vyao wanavyo kaa ili kuweza kupata mradi mmoja wenye tija kwa Wananchi kuliko kuwa na miradi mingi ambayo haitekelezeki.
Amesema ni vyema kuwa na mradi katika eneo moja na kuchagua kata moja ambayo watajenga mradi mkubwa na utakaowafanya wananchi kufika kwa urahisi ili kupatiwa huduma.
"'Niwapongeze viongozi wa Manispaa kazi inaonekana fedha kidogo kazi kubwa , kwakweli mradi huu tutautangaza kwa Mhe. Rais Dkt . John Magufuli kuonesha jinsi gani mlivyokuwa makini katika matumizi ya fedha, pia niwaombe najua kila Diwani wa Kata angetamani kuwa na mradi ndani ya kata yake lakini ni vyema mkawa na kipaumbele cha kuweka mradi katika kata moja tu ambayo mtaona wananchi wanaweza kufika kwa urahisi kuliko kuwa na miradi mingi isiyotekelezeka," Amesema Mhapa.
Hata hivyo, amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, kuhakikisha mara baada ya kukamilika kwa mradi wa Soko kuu la kisasa waweke uongozi mzuri ambao wataamua katika Baraza lao na utakaokuwa unauwezo wa kukusanya fedha ili Manispaa iweze kuendesha miradi mingine.
Amesema siku zote rasilimali pesa inakuwa ndogo kuliko idadi ya watu, hivyo wajifunze katika miradi ya wenzao kuona wanaendesha soko vizuri, isje tena mkawa mmeleta mradi harafu mradi huo ukaleta migogoro na kutokuwa na tija kitu ambacho hakitawasaidia katika kufikia malengo yao ya kukusanya kodi.
Katika hatua nyengine, ameutaka Uongozi wa Halmashauri kuhakikisha wanaweka viwango vya bei rafiki na nafuu kwa Wafanyabiashara ili waweze kufanya biashara katika kupata vipato vyao na Halmashauri kuingiza mapato.
Katika hatua nyengine, ameipongeza Manispaa kwa kupata hati safi kwa kipindi cha miaka 6 mfululizo, hivyo amewaambia kupata hati safi sio jambo jepesi hii inaonesha ni jinsi gani Mkurugenzi, Meya pammoja na waatalamu wake walivyo na ushirikiano katika kuijenga Manispaa hiyo.
Amesema Mhe. Rais Dkt John Magufuli hanaga utani katika fedha anazozitoa katika miradi , hivyo anataka kuona pesa anazozitoa zinatumika kwa miradi iliyokusudiwa na kuleta tija kwa Wananchi na kuona watu wa chini wananufaika na miradi hiyo.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa ALAT, Elirehema Kaaya, ameitaka Halmashauri kuhakikisha Soko hilo linatumika vizuri ili wale waliokusudiwa kuingia katika Soko wawe wakwanza kuingia.
"" Nikuombe Mkurugenzi pamoja na Mstahiki Meya nategemea Soko likiisha kuwepo na amani nawaamini sana , asipatikane mtu yeyote akajipatia kipato kupitia mgongo wa nyuma, nataka kila anayeingia katika soko hili awe mfanyabiashara, mnajua tunavyoumia sasa endeleeni kusimamia jengo liishe salama na muwakee wamamchinga pamoja na Mama lishe maeneo yao ya biashara hawa ni marafiki wa Mhe. Rais John Pombe Magufuli, Mhe. hataki kuona watu wanakula kupitia jasho la mtu fanyeni kazi ili tupate pesa za kuendesha miradi mingine kwani mradi huu ni chanzo kikubwa cha pesa za ndani " Amesema Kaaya.
Pia amefurahishwa zaidi kuona Watu wenye uhitaji maalumu wametengewa maeneo yao maalumu, jambo ambalo linalenga kuleta usawa kwa wote na kuendeleza adhima ya Mhe. Rais ya kuwaendeleza Walemavu , Wakina Mama pamoja na Vijana.
Hata hivyo, amempongeza Mkandarasi pamoja na Mhandisi wa Manispaa kwa kazi nzuri na kuwataka wote kwa pamoja waongeze umakini zaidi ili mradi huo ukamilike kwa wakati na uwanufaishe wananchi.
Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, ameupongeza Uongozi wa ALAT Taifa kwa kutembelea mradi wa Soko kuu la kisasa na kujua maendeleo yake.Amesema Manispaa imekuwa ikitembelea mradi huo mara kwa mara katika kuona mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Aidha amesema atahakikisha mara baada ya kukamilika kwa mradi huo, wafanyabiashara waliosaini mikataba ya awali kabla ya ujenzi kuanza ambao walikuwa katika Soko la zamani wanapewa kipaumbele kufanya biashara katika soko hilo.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, ameishukuru ALAT na kusema wamefanya jambo zuri kutembelea mradi huo kwani wameanzia Mkoa wa Iringa na sasa wapo Mkoani Morogoro hii inaonesha mabadiliko makubwa kwa upande wa ALAT.
Amesema, kitendo cha ALAT kutembelea miradi mbali mbali kinasaidia kuzimulika Manispaa na kuonesha jinsi utekelezaji wa miradi inavyotekelezwa.
.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa