MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe.Balozi Dkt. Batilda Buriani leo Agosti 2, 2024 amezindua Sherehe za Maonesho ya Wakulima – Nane Nane Kanda ya Mashariki inayojumuisha mikoa ya Dar Es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro na kutembelea mabanda mbalimbali ya maenesho katika katika Viwanja vya Kambarage Nyerere Nanenane Mkoani Morogoro.
Akifungua maonesho hayo, Balozi Batilda, amewashauri wakulima,wavuvi na wafugaji kutumia vyema fursa ya maonesho ya wakulima ya Nanenane, kujifunza teknolojia mpya na ya kisasa ambayo itawasaidia kupata tija katika shughuli zao za kilimo, mifugo na uvuvi.
Balozi Dkt. Batilda,amesema asilimia 65 ya Watanzania wamejiajiri kupitia sekta ya kilimo, ambacho inachangia asilimia 28 ya pato la taifa, hivyo kuwataka kuongeza juhudi katika kujifunza teknolojia mbalimbali za kisasa ili sekta hiyo iweze kuchangia pato la taifa kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2030.
“Tunategemea baada ya uzinduzi huu kuona wananchi wengi kutoka kwenye kanda zetu wanakuja kujifunza shughuli mbalimbali zinazofanyika katika haya maonesho,” Amesema Dk. Buriani.
Aidha, amesema kuwa maonesho hayo yana lengo la kutoa elimu kwa wananchi ili kuongeza mnyororo wa thamani kwa wakulima, wafugaji, wavuvi pamoja na wadau wengine sambamba na kuongeza tija na ufanisi katika shuguli wanazozifanya.
Amesema kuwa mikoa hiyo ya Kanda ya Mashariki inakila sababu ya kufanya vizuri katika sekta ya Kilimo kutokana na uwepo wa ardhi nzuri yenye rutuba, hali ya hewa nzuri pamoja na vyanzo vingi vya maji na kwamba wakulima kufanya hivyo kutaongeza usalama wa chakula pamoja na lishe.
Sambamba na hilo, Dk. Batilda ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wafugaji kufika katika maonesho hayo ili waweze kuona na kujifunza namna bora ya kupanda malisho na kuacha ufugaji wa kuhama hama ambao husababisha migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
“Na huu ufugaji tunaozungumzia hapa sio ule wa kuhama hama, katika maonesho yetu tunawaonyesha wafugaji aina za malisho kama majani ya aina tofauti yenye virutubisho vya aina mbalimbali ili wafugaji wetu waanze kufuga kisasa, tunataka tutokane na migogoro inayotokana na ufugaji holela,”ameeleza.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa