BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro limewataka Wataalam wa Manispaa kuhakikisha wanatoa maelekezo ya michoro yao mapema kabla hawajaanza utekelezaji wa miradi ili iwe na tija kwa wananchi.
Hayo yamezungumzwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Pascal Kihanga, wakati wa Mkutano wa Kawaida wa Baraza la Madiwani ulilofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya Morogoro Januari 30,2020.
Akizungumza na Waandishi wa habari, amesema Baraza hilo halina shida ya kugombana na Timu ya Wataalamu wa Manispaa lakini kikubwa wangependa kupatiwa maelekezo ya kina kutoka kwa Wataalam juu ya miradi wanayokwenda kuitekeleza ili kushauriana na kuangalia ni jinsi gani miradi hiyo itakavyokuwa na tija kwa Wananchi.
Aidha, amewataka Wataalam kufanya kazi kwa pamoja na pale wanapokwama walishirikishe Baraza ili waone jinsi ya kuweza kukwamuana mahala ambapo panaonekana kuna tatizo au panahitaji maelekezo ya kina.
"Niwaombe Wataalam , msiwaone Madiwani wanalalamika na kupiga kelele, hii yote ni kutaka kujua miradi inavyoendelea na kuleta tija kwa wananchi maana hata hizo pesa zinazotumika ni kodi za Wananchi hivyo ni lazima wajue na kufuatilia ili wao wawe mabalozi wazuri wa kuizungumzia miradi hiyo katika vikao vyao na kama tutashirikiana kwa pamoja maendeleo ya Manispaa yetu yatazidi kuwa juu" Amesema Mhe. Kihanga.
Amesema maendeleo ya Manispaa ya Morogoro ni ya wote hivyo Manispaa wakifanya vizuri Mkurugenzi, Baraza la Madiwani , Watumishi, Wakuu wa idara na wananchi wote watasifiwa.
Katika hatua nyengine, akijibu swali la Diwani Viti Maalum Kata ya Kiwanja cha Ndege, Mhe. Doroth Mwamsiku lililouliza mikutano ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi ni endelevu au kwa muda mfupi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheilla Lukuba, amesema mikutano hiyo ya hadhara ni endelevu hivyo mpango uliopo ni kushuka Mtaa kwa Mtaa kufuatia agizo la Mhe. Rais la kutaka Manispaa na Wilaya kushuka chini kusikiliza wananchi.
Amesema lengo la ziara hiyo ni kusikiliza na kutatua kero za Wananchi ili kurahisisha huduma kwa jamii pamoja na kufahamu kuhusu miradi mbali mbali inayotekelezwa na kero zilizotatuliwa katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM chini ya Rais wa awamu ya tano, Mhe Dkt John Pombe Magufuli.
Katika kikao hicho pia kulikuwa na maswali ya papo kwa papo ambapo Diwani wa kata ya Mji Mpya, Mhe. Wenslaus Kalogeries, amesema katika Soko la Mji mpya kuna mfereji mikubwa imechimbwa lakini haina mwendelezo mzuri pamoja na kuwepo kwa uharibifu wa barabara kipindi kilichonyesha mvua na kutaka kujua changamoto hizo zinatatuliwaje na mamlaka husika.
Kuhusu uendeshaji wa Soko, Sheilla, amesema suala hilo wamekuwa wakilijadili katika vikao lakini wanatarajia kulifikisha katika kwenye kikao cha fedha cha mwezi wa pili na Baraza la Madiwani kwani wao ndio wenye wananchi na kuona jinsi gani watapanga kwa ajili ya maslahi ya maendeleo ya Manispaa na wananchi kwa ujumla bila kuathiri mambo mengine na kufanya Soko hilo kuwa na tija.
Akijibu swali hilo, Meneja wa TARURA Manispaa ya Morogoro, Mhandisi James Mnene, ni kweli wakati wa mvua zinanyesha walikusanya taarifa ya barabara zote zilizoharibika na kuzipeleka TARURA Mkoa kwa ajili ya kuweza kupatiwa fedha za dharura ili kuanza matengenezo ya barabara hizo huku akisema suala la mtaro uliochimbwa kupisha barabara yenye urefu wa Mita 670, mtaro huo ulichimbwa kufuatia kukumbwa na changamoto ya maji (water table) lakini walimkata mkandarasi wa barabara hiyo jumla ya shilingi milioni 28 baada ya kuchelewa kushughulikia suala hilo la mitaro na taarifa zilipelekwa TARURA Makao makuu ili kupata fedha hizo lengo likiwa ni kujenga mtaro huo kwa mawe na kuleta ubora.
Katika hatua nyengine, Diwani Kata ya Kihonda, Mhe. Hamisi Kilongo, ameuliza swali la kujengwa kwa majengo mafupi katika Stendi mpya ya Daladala iliyopo Mafiga kufuatia mapendekezo ya kamati ya Fedha, huku Meneja wa TARURA , Eng. James Mnene amesema majengo hayo yalijengwa kwa kuzingatia dizaini na ushauri kutoka kwa Mshauri wa mradi huo na kusema yatakapokamilika hayatakuwa na shida.
Kwa upande wa Mhandisi wa Manispaa ya Morogoro, Juma Gwisu, amesema Mapaa ya majengo yamezingatia vigezo vya eneo husika hivyo kama yatabadilishwa yatakuwa na athari zake.
Kuhusu Ujenzi Holela, Afisa Ardhi wa Manispaa ya Morogoro, Gisbert Msemwa, amesema katika mwaka wa fedha 2020/2021 wameweka maombi ya kupata Bodaboda 4 kwa ajili ya kusaidia kuzunguka katika maeneo yaliyopo katika Manispaa na kufanya ukaguzi wa ujenzi holela unaofanyika.
Amesema kwa sasa idara hiyo ina wataalam 11 na wanatakiwa wataalam 72 ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu lakini kikubwa ni ushirikianao kwa Madiwani, Wananchi ili kuweza kusaidia katika kukomesha ujenzi holela.
Pia amewataka Viongozi kuanzia ngazi za Mitaa na Kata wanapofanya mikutano na wananchi wawaite na kuiweka agenda ya Ujenzi holela iwepo katika kila mikutano hiyo ili waweze kuendelea kutoa elimu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa