BARAZA la Madiwani Manispaa ya Morogoro imeidhinisha kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 101,091,069 katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Kauli hiyo imetolewa Machi 01/2024 na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la kupitisha mpango na Bajeti ya Manispaa ya Mwaka 2024/2025 uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano Ofisi Kuu ya Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza katika Baraza hilo, Mhe. Kihanga, amesema ,matumizi hayo yamepanda kwa asilimia 17.11 ya matumizi ya mwaka wa fedha 2024/2025ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 ya shilingi Bilioni 83,792,226,268.00.
Mhe. Kihanga, amesema Bajeti hiyo itasaidia kuwaletea wananchi maendeleo ikiwa pamoja na kuongeza na kuboresha miundo mbinu ya huduma za kijamii kama vile huduma za Sekta ya Elimu,Huduma za Afya, Maendeleo ya jamii, miundombinu ya barabara na Mazingira.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kihanga, ametakaWatumishi wazingatie maelekezo ya Waheshimiwa Madiwani katika kusimamia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo na kuzingatia vipaumbele vya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kwa lengo kuu la kuwaletea maendeleo Wananchi wa Manispaa ya Morogoro Pamoja na kutoa huduma bora.
“Baraza la Madiwani lina wajibu wa kusimamia mapato ya ndani kwa maslahi mapana ya Wananchi na kuhakikisha kuwa mstari wa mbele katika kuhoji matumizi ya mapato hayo ili kuepusha upotevu wa mapato kwa namna yeyote ile, hivyo hivyo Watendaji wa Kata mnatakiwa kusimamia na kutumia kikamilifu fedha za Miradi ya Maendeleo katika Kata zenu na kuwa na mpango kazi wa matumizi wa fedha hizo za miradi ya maendeleo jinsi mnavyosimamia “ Amesema Meya Kihanga.
Akiwasilisha rasimu ya Bajeti ya mwaka 2024/2025,Afisa Mipango wa Manispaa ya Morogoro kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa , Jeremiah Lubereje, amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 mapato ya ndani ya Manispaa yalikuwa ni shilingi Bilioni13,185,280,000.00.
Lubereje,amesema kwa mwaka ujao wa fedha 2024/2025 Manispaa ya Morogoro inategemea kukusanya jumla ya sh Bilioni 15,622,877,022.05 katika mapato ya ndani.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro , Ally Machela, amesema Bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 utekelezaji wake utakuwa madhubuti katika ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na fedha zinazotoka Serikali kuu kwaajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo kwa maslahi makubwa ya Wananchi.
Machela, amesema Bilioni 7,832,732,718.6 sawa na 60% zitatumika katika miradi ya Maendeleo, na Bilioni 5,221,821.40 zitaelekezwa kwa matumizi ya kawaida na milioni Tsh 59,388,000.00 zitatumika kwaajili ya mishahara ya watumishi wanaolipwa kupitia mapato ya ndani.
Kwa upande wa Mkuu wa wilaya ya Morogoro Mhe. Rebecca Nsemwa, ameupongeza uongozi wa Watumishi wa Manispaa ya Morogoro kwa kuandaa bajeti yenye kusimamia vigezo vyote vya mahitaji ya Wananchi kwa kusimamia IIani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwasisitiza kuisimamia vyema katika utekelezaji ili kumwakilisha vyema Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
DC Nsemwa, ameipongeza Menejimenti ya Manispaa ya Morogoro chini ya Mkurugenzi wa Manispaa, Ally Machela kwa kuandaa vizuri bajeti ambayo itakwenda kusaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto za wananchi.
“Wataalamu wetu mmeitendea haki sana hii bajeti hongereni sana lakini niwapongeze pia Madiwani wetu kwa usimamizi Madhubuti na imara wa miradi ya maendeleo , wananchi wana mategemeo makubwa na sisi, tuwatumikie kwa kusimamia vyema fedha za miradi ili kupata matokeo chanya, tunatarajia kuwa Jiji , hatuwezi kuwa Jiji kama tutashindwa kusimamia miradi ya maendeleo , tushirikiane kwa pamoja kuijenga Manispaa yetu na kutekeleza Ilani ya CCM na yale maagizo yote kutoka Serikali Kuu chini ya mama yetu kipenzi Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan” Amesema DC Nsemwa.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Morogoro Mjini ,Fikiri Juma, amesema bajeti ya mwaka 2024/2025 inakwenda kuakisi utatuzi wa changamoto za wananchi.
Aidha ameleza kuwa ipo haja katika upade wa Sekta ya Miundombinu, Uongozi wa Manispaaa ya Morogoro kuwa na kikao cha pamoja cha kujadili hali ya miundombinu ya barabara kwa Kata zote ambazo zina changamoto ya barabara ili kupata utatuzi wa pamoja.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa