MANISPAA ya Morogoro inatarajia kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 19, 606,559.46 kutoka Serikali Kuu kutekeleza mradi ya Tactics utakaosimamiwa na mtaalamu mshauri wa miradi kutoka kampuni ya ujenzi ya MHANDISI (Consultancy) LTD, na kutekelezwa chini ya Kampuni ya ujenzi ya M/s Jiangxi Geo-Engineering (Group) Corporation.
Akizungumza katika utambulisho wa mradi huo tarehe 23.10. 2023 kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi Kuu ya Manispaa , Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, ndugu Winfred Kipako, amesema Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa Halmashauri 12 zinazotekeleza mradi wa TACTICS nchini, kwa awamu ya kwanza, na kwamba Manispaa itanufaika na mradi huo kwa ujenzi wa barabara za lami nzito zenye urefu wa KM 20.59, katika maeneo ya Muhimbili, Tubuyu II, Mjimwema, Barakuda na Kihonda-VETA, vilevile kutakuwa na ujenzi wa mifereji ya maji ya (ANT Mlaria na Kikundi), itakayosaidia kuondoa adha ya mafuriko katikati ya mji.
Vilevile, ndugu Kipako amewataka wakandarasi na mtaalamu mshauri wa mradi huo kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi na kwa uzalendo kwa manufaa ya wana Morogoro huku akiwataka wananchi wa Manispaa ya Morogoro kuwajibika ipasavyo katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa ubora, kwa kipindi chote cha utekelezaji waa mradi.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro Mheshimiwa Pascal Kihanga, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu mkubwa ambao unakwenda kuifungua zaidi Manispaa.
“Niombe wananchi ambao mtapisha ujenzi huu, mara mpatapo malipo yenu mpishe kwa wakati ili mradi uende kadri ulivyo pangwa lakini wananchi niombe mlinde na kuitunza miundombinu ambayo Serikali inawekeza kwa fedha nyingi” Amesema Mheshimiwa Kihanga.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Morogoro, ndugu Jeremiah Lubeleje, amewaomba TANESCO, MORUWASA na TTCL kuwa na mpango mkakati wa haraka wa kuondoa miundombinu ambayo itapitiwa na mradi ili utekelezaji ukamilike kwa wakati.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa