Mkuu wa Wilaya ya Morogoro , Regina Chonjo amemua kusimamia kidete misingi ya utawala bora unaoheshimu sheria kwa kuwaondoa wafanyabiashara wadogo (Machinga) kufanya shughuli zao kati kati ya mji pembezoni mwa barabara baada ya kuacha masoko yao waliyotengewa rasmi.
Chonjo alisema hayo katika hotuba yake wakati alipoalikwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Morogoro kilichofanyika hivi karibuni mjini Morogoro chini ya Meya wa Manispaa Pascal Kihanga.
Mkuu huyo wa wilaya alisema, hata kama atakuwa ameuweka ukuu wake wa wilaya rehani lakini hataki kuona uvunjwaji wa sheria kwa kuwa tayari wafanya biashara hao wametengewa maeneo ya kufanyika bishara zao.
Pamoja na kutengewa maeneo hayo alisema , cha kusikitisha wamekaidi na kuhamia kati kati ya mji pembezoni mwa barabara na kusababisha kero kwa watumiaji wengi wa barabara hizo ambao nao wanahaki ya kuzitumia.
Alisema , pamoja na watu kusema nimeuweka ukuu wangu wa wilaya rehani , kwangu kinachotakiwa ni kila mmoja kufuata utaratibu na sheria zilizipo, hivyo sitakuwa tayari kuona watu wakifanya mambo kwa kujiamlia wao wenyewe.
Chonjo alisema , lengo lake ni kutaka kuona Manispaa ya Morogoro inakuwa mji safi , hivyo kitendo cha wafanyabiashara hao kuendelea kufanya shughuli zao kati kati ya mji ni moja ya sababu zinazochangia Manispaa kuwa kwenye hali ya uchafu kutokana na mitaro mingi kugeuzwa madampo ya kutupa uchafu.
Mkuu huyo wa wilaya alisema , kauli ya Rais Dk Magufuli ya kuwataka wafanya biashara hao maarufu ‘ Machinga’ waruhusiwe kufanya kazi zao mjini imetafsiliwa vibaya na kusababisha baadhi kuyahama masoko waliyokuwa wakifanya shughuli za biashara na kuhamia mitaani kati kati ya mji.
Hata hivyo alisema , baadhi ya wafanyabiashara walitumia mwanya huo na kuacha meza zao sokoni na kuhamia katikati ya mji pembezoni mwa barabara huku wakiwa na magunia mbalimbali ya bidhaa zao.
Alisema , wanafanyabiashara wanaoruhusiwa ni wale wanaotembeza bidhaa zao wakitafuta wateja na siyo kuweka bidhaa zao pembezoni mwa barabara ambapo alisisitiza kuwa yeyote atakayekamatwa atafikishwa kwenye vyombo vya kisheria.
Hata hivyo kutokana na agizo la kuwaondoa wafanyabiashara wote waliovamia katikati ya mji, mkuu wa wilaya aliwataka Madiwani wa Manisapaa kumpa ushirikiano kwani lengo ni kutaka kuona Manispaa inakuwa Jiji lenye ufahari wake.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Morogoro , Kihanga alisema kuwa, kitendo cha kuwaondoa wafanya biashara hao kinaungwa mkono na Madiwani wote ambapo alitahadhalisha kitendo hicho kisitumike kisiasa.
Wafanyabiashara hao kabla ya kuhamia kufanyia biashara pembezoni mwa barabara walikuwa katika masoko ya Chamwino, Mwembesongo ,Madizini ,Kihonda Maghorofani na Kichangani ambayo yameachwa wazi na hivyo kutakiwa kurudi kwenye masoko yao ya zamani .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa