Maafisa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi Ndogo Inayoratibu Miradi Inayofadhiliwa na Benki Kuu ya Dunia na Wafadhili Wengine, leo tarehe 02.02.2024 wamefanya kikao na Kamati ya Wataalamu ya Halmashauri ya Manispaa Morogoro (CMT), kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu kipengele kingine cha Mradi wa Kuboresha Miji (TACTIC), kinachojumuisha kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri, mipangomiji, masuala ya majanga, kuzalisha ajira mpya kupitia rasilimali zilizomo ndani ya Manispaa, na udhibiti wa taka ngumu.
“Sisi leo tumekuja kukutana nanyi ili tuwafahamishe zaidi juu ya utekelezaji wa TACTIC ili mwe tayari na mjiandae kwa kuainisha mambo ambayo mnaona yakifanyika basi matokeo ya mradi huu yatakuwa mazuri sana kwa manufaa ya sasa na ya baadae, kwa wananchi, Manispaa na nchi kwa ujumla” alieleza mmoja wa maafisa hao, ambaye kwa cheo yeye ni Afisa Mipangomiji.
“Kipengele cha ujenzi wa miundombinu tayari kimeshaanza kutekelezwa na leo hii tumekuja kwa ajili ya kipengele cha usimamizi wa miji ambapo tunataka ninyi (menejimenti) mtuambie yale ambayo mnafikiri yakifanyika yataimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, mipangomiji, yatazalisha ajira mpya na kudhibiti taka ngumu” alieleza Afisa mwingine.
Naye mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu ya Manispaa ya Morogoro, ambaye pia ndiye Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, ndugu Ally Machela amewashukuru maafisa hao akisema kupitia kikao hicho yeye binafsi amebaini kwamba menejimenti inayo kazi kubwa ya kufanya `katika utekelezaji wa mradi wa TACTIC, pia anaamini kwamba uelewa wa timu yake kuhusu TACTIC sasa umeongezeka zaidi kutokana na maelezo waliyoyawasilisha leo maafisa hao.
“Kupitia kikao hiki ninaona kwamba menejimenti imeongezewa uwezo mkubwa katika ushiriki wake kwenye utekelezaji wa mradi huu hivyo itabidi baada ya kikao hiki tukae na kuainisha mambo yote muhimu ambayo tunataka yafanyike kwenye Manispaa yetu wakati wa utekelezaji wa mradi” alieleza Machela.
Mradi wa TACTIC unalenga kuboresha utoaji huduma kwenye miji, unatekelezwa kwenye miji 45 nchini ikiwemo Manispaa ya Morogoro, na utekelezaji wake upo katika vipengele vinne ambavyo ni kuimarisha usimamizi wa miji, kujenga miundombinu ya kimkakati, usimamizi wa mradi, na kipengele cha nne ni kuhusu wanufaika wa mradi, ambao ni wananchi.
MWISHO
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa