HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na Dawati la ukaguzi wa Kijinsia Mkoa wa Polisi wa Morogororo pamoja na Kituo cha Msaada wa Sheria Morogoro wameungana kusherekea maadhimisho ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Maadhimisho hayo yamefanyika Novemba 25, 2019 kwenye Viwanja vya Kilakala Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, Mkaguzi wa Polisi Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Polisi wa Morogoro, Sophia Ngoso, amesema maadhimisho hayo ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia hufanyika kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Desemaba 12 yakiwa na lengo la kuzungumzia masuala mbali mbali yanayohusu ukatili katika Jamii.
Amesema kwa upande wa Morogoro, wameadhimisha maadhimisho hayo na kongamano ikiwamo kucheza mechi kati ya Waendesha Boda boda na Bajaji kwani lengo la kuwakutanisha ni kutaka kupata ushirikiano baina ya Wanaume na Wanawake .
Aidha amesema siku zote wamekuwa wakiegemea kuwapatia elimu Wanawake na Watoto huku wakiwasahau wanaume ambapo kwa upande wake amesema wanaume ndio kichochezi kikubwa cha ukatili wa Kijinsia katika Jamii.
"Tumeamua kuwakutanisha wanaume hapa kwani tunawasahau sana , ukiangalia katika takwimu yetu wanaume, Dereva wa Boda boda na Bajaji wanaongoza katika kufanya vitendo vya ukatili wa kijinsia, hivyo tumeitana ili tupeane mikakati thabiti na kuwafanya kuwa mabalozi wazuri na kuondoa ukatili huu ndani ya familia na nje ya jamii inayomzunguka " Amesema Bi. Ngoso.
Pia ameeleza kuwa anategemea baada ya maadhimisho hayo jamii itakuwa na uelewa mpana juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia, na jamii itaishi huru bila ukatili wa kijinsia huku akisema hawatamvumilia mtu yeyote atakayefanya ukatili wa kijinsia.
Naye Nahodha wa Timu ya Bodaboda, John Luhembe, amesema mafunzo yaliyotolewa yatawasaidia sana hususani katika vikundi vidogo vidogo vya wananchi wataweza kuwa mabalozi wema wa kusimamia misingi ya sheria na kanuni pamoja na kuifuata katiba ya Jamhuri ya Muungano na kuacha tabia ya kufanya vitendo vya ukatili wa Kijinsia.
"Siyo boda boda wote wanajihusisha na ukatili wa kijinsia lakini wakati mwengine hali hii inatokana na ugumu wa maisha, kwani unakuta mwanafunzi anatoka nyumbani mzazi hampi pesa ya kula hivyo akiwa anapakiwa na boda boda anaweza kumlaghai, lakini watakaa na boda boda kwa ajili ya kupeana elimu kwakuwa boda boda wanalalamikiwa sana katika ukatili wa kijinsia kwa Wananafunzi" Amesema Luhembe.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa