Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Regina Chonjo amewasisitiza wadau kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha,kuchagua viongozi walio bora katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 24/11/2019.
Chonjo ameyasema hayo wakati wa kikao cha wadau wa Uchaguzi na kueleza kuwa Serikali za mitaa zimeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 145 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 hivyo uchaguzi wa Serikali za mitaa ufanyika kila baada ya miaka mitano kwa kuzingatia matakwa ya sheria.
Aidha alieleza kuwa Manispaa imejipanga kuendesha uchaguzi katika mazingira ya haki na usawa kwa kuzingatia misingi ya uhuru wa kidemokrasia hivyo aliwasisitiza wadau kuwa mabalozi wazuri kuelimisha wananchi juu ya kujiandikisha na kupiga kura na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kuweza kupata viongozi bora watakaosaidia kufanikisha jitihada za Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe.Dkt John P.Magufuli.
Naye msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Morogoro mjini Ndg Waziri Kombo ameeleza kuwa uandikishaji wa wapiga kura utaanza kuanzia tarehe 8/10/2019 hadi 14/10/2019 na vituo vitafunguliwa kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
Kombo amebainisha sifa za mpiga kura kuwa anatakiwa kuwa raia wa Tanzania,awe na umri wa kuanzia miaka kumi na nane au zaidi,awe hana ugonjwa wa akili,na awe amejiandikisha kupiga kura katika mtaa husika.Aidha ameeleza mwananchi atakosa sifa za kupiga kura endapo atakosa sifa zilizobainishwa na endapo atakuwa amejiandisha kupiga kura katika kituo zaidi ya kimoja.
Aidha Kombo ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kuchukua fomu za kugombea zitakazotolewa tarehe 29/10/2019 hadi 4/11/2019 na uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 5/11/2019.
Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ina tarafa moja na kata 29 na inatarajia kuwa na wapiga kura 177,000,na kila mtaa utakuwa na kituo cha kuandikisha na kupigia kura ambavyo vitapatikana katika majengo ya umma na maeneo ya wazi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa