Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo,amekabidhi jumla ya Ndoo 100 za kuwekea maji tiririka pamoja na sabuni ikiwa ni jitihada za kujikinga na Ugonjwa wa CORONA Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza na Waandishi wa habari, amesema kuwa ndoo hizo zimenunuliwa chini ya ufadhili wa Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini,Mhe. Abdulaziz Abood katika kuhakikisha Wananchi wa Jimbo lake wanajikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Amesema kuwa ni jukumu la Wananchi kuzitunza ndoo hizo ili ziendelee kutumika katika maeneo yao ya biashara.
Aidha, amesema Ndoo hizo sio mali ya mtu binafsi bali kila mtu atakuwa na haki ya kuitumia ili kuweza kusaidia katika kujikinga na Maambukizi ya Virusi vya CORONA COVID -19.
“Leo tunagawa Ndoo hizi katika maeneo tofauti tofauti, kikubwa niwaombe Wananchi kwamba wawe wastaarabu katika kuvitunza isitokee mtu akakichukua akajifanya ni ya kwake, Mhe. Wenu Abood anawapenda sana , katika kuona janga hili linakuwa halina madhara ameona ni vyema akaungana na Wananchi wake kuwasidia ili katotumia ile pesa ambayo ni mitaji yenu msiitumie badala yake ametoa ndoo hizi na sabuni, kikubwa elimu iendelee kutolewa na sisi wenyewe tuwe mabalozi wazuri wa kuelimishana juu ya kujikinga na Ugonjwa huu ambao ni hatari sana ukiangalia Mataifa ya wenzetu wanateketea sana hivyo lazima na sisi tuchukue tahadhari kubwa ya kujikinga ili tuwe salama”Amesema DC Chonjo.
Kwa upande wa Mwananchi, Juma Abdallah, amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Morogoro pamoja na Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdulaziz Abood kwa kuwapatia ndoo na sabuni.
“Tunawashukuru sana Viongozi wetu kwa kuonesha moyo wa kutujali sisi katika vijiwe vyetu tumekuwa tukipeana sana elimu lakini ujio wako tena kwa kutupatia vifaa kama hivi umetufariji sana, sasa tunaungana na Serikali yetu kupaza sauti kwa pamoja ili kuhakikisha kila mwananchi anajikinga na ugonjwa huu na kufanya Taifa letu kuwa salama hususani katika Manispaa yetu ya Morogoro” Amesema Juma.
Pia amechukua nafasi ya Kupongeza Jitihada zinazofanywa na Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro chini ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Sheila Lukuba pamoja na Mganga Mkuu wa Manispaa ya Morogoro , Dr Ikaji Rashid na timu nzima ya Wataalamu wa Afya kuanzia Ngazi ya Wilaya, Manispaa na Kata hadi kwenye Mitaa kwa jitihada kubwa za kutoa elimu dhidi ya kujikinga na Ugonjwa wa CORONA.
Miongoni mwa maeneo ambayo ndoo hizo zilisambazwa ni pamoja na Stendi ya Daladala Mjini, Stendi ya Bajaji (Jumata) na Wauza Matunda, Soko la Manzese na Vijiwe vya Bodaboda, Soko la Fire Kiwanja cha Ndege, Masika, Stendi ya Daladala Kaloleni, Stendi ya Mabasi Msamvu na maegesho ya Magari ya kukodishwa nje ya Stendi ya Msamvu, Kihonda viwandani, Mazimbu Road, Kihonda kwa Chambo, Barabara ya Ipo Ipo, Soko la Mazimbu jirani na Ofisi ya Kata ya Mazimbu, Chamwino pamoja na Soko la Chamwino.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa