MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Regina Chonjo, amewataka Maafisa Tarafa wa Wilaya ya Morogoro kutoa taarifa na takwimu halisi ndani ya masaa 24 kuhusu vitambulisho walivyokabidhiwa vya Wajasiriamali na taarifa zifikishwe kwa Katibu Tawala wa Wilaya kesho Tarehe 20 , 2020 saa 2:00 Asubuhi .
Hayo ameyasema leo Februari 19,2020 Ofisini Kwake kufuatia kikao alichokiitisha dhidi ya Maafisa Tarafa juu ya utoaji wa taarifa ya ugawaji wa Vitambulisho kwa Wafanyabiashara wadogowadogo Wilaya ya Morogoro hadi kufikia tarehe 14,Februali 2020.
Aidha ametoa taarifa na takwimu kwa Tarafa zilizokabidhiwa Vitambulisho hivyo ambapo jumla ya Tarafa saba zilizopo ndani ya Wilaya ya Morogoro zilikabidhiwa Vitambulisho hivyo kufuatia kauli iliyotolewa na Serikali kwamba Wakuu wa Wilaya wawakabidhi zoezi hilo Wakurugenzi wa Manispaa.
Amesema taarifa zinazotakiwa kuwasilishwa katika Ofisi yake ni pamoja na vitambulisho vilivyokabidhiwa Wilayani, Vitambulisho vilivyokabidhiwa katika Tarafa, Vitambulisho vilivyouzwa vikionesha thamani ya pesa, Vitambulisho fedha zake zilizopelekwa benki, fedha ambazo hazijapelekwa benki pamoja na Vitambulisho vilivyobakia.
Katika taarifa aliyoisoma kupitia tarafa zote 7 za Wilaya ya Morogoro, zimeonesha kuwa Tarafa ya Manispaa ilikabidhiwa vitambulisho 13,146 vyenye thamani ya Tshs 262,920,000.00 na kuuza vitambulisho vyote ambapo jumla yake ni Tshs 262,920,000.00 sawa na asilimia 100, Tarafa ya Mikese walipewa vitambulisho 900 thamani ya Tshs 18,000,000.00 na kuuza 853 kwa shilingi 17,060,000.00 sawa na asilimia 94.78 na kubakiza 37, Tarafa ya Mvuha walipewa vitambulisho 570 vyenye thamani ya tshs 13,000,000.00 na kubakiza 71, Tarafa ya Bwakila vitambulisho 830 na kuuza 772 vilivyobaki ni 34, Tarafa ya Ngerengere walipewa vitambulisho 998, kuuza 903 na vilivyobaki 90, Tarafa ya Mkuyuni vitambulisho 1100, waliuza 822 na kubakia 278 pamoja na Tarafa ya Matombo ambao walipewa vitambulisho 950, kuuza 788 na kubakia na 147.
Aidha, amesema katika Wilaya ya Morogoro, Vitambulisho vya Wajasiriamali wadogowadogo vilivyokabidhiwa kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro mwaka 2019 vilikuwa 18,500 ambapo awali zoezi hilo lilikuwa likisimamiwa na Wakuu wa Wilaya kabla ya kulishusha kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa.
Katika hatua nyingine, amewataka Maafisa Tarafa wahakikishe ifikapo kesho Saa 2:00 asubuhi taarifa zote za Vitambulisho vya Wajasiriamali ziwe zimewasilishwa kwa Katibu Tawala wa Wilaya ili aweze kuzikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa Mhe. Olata Sanare kwa mujibu wa maelekezo waliyopatiwa.
"Tusifanye mchezo , nataka kesho mapema muanze leo kuwasumbua hao watendaji wenu taarifa hizi tulishatoa na mwisho ni kesho Februali 20,2020 pamoja na kutoa muda mrefu mkaona kama utani sasa kesho nazitaka na pesa hizi za Mhe. Rais Dkt John Magufuli haziliwi na kama wapo waliozila watazitapika adhabu yake ni Mahakamani na hakuna dhamana zaidi ya kurudisha pesa hizo, mmepewa dhamana nataka kazi hiyo ifanyike leo hii mpaka saa 12 jioni muwenazo taarifa zote "Amesema DC Chonjo.
Hata hivyo amewataka Maafisa Tarafa kufanya kazi kwa kutambua majukumu yao na nguvu waliyonayo ili kuwaletea Wananchi maendeleo ikiwemo kutatua kero za wananchi kwa kupanga vipaumbele vyao katika maeneo wanayoishi.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa