Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo amelazimika kuwafuata wajasiriamali wadogo katika maeneo yao ya biashara ili kuwapatia elimu ya kutosha kuhusu faida ya kuwa na kitambulisho cha mfanyabiashara mdogo baada ya kubaini wengi wao hawajahamasishwa vya kutosha ya kutambua manufaa watakayopata.
Chonjo alisema hayo katika hotuba aliyoitoa kwenye kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Morogoro baada ya kualikwa kutoa salamu za serikali ya wilaya nakutumia fursa hiyo kuwahimiza madiwani kushiriki kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo katika kata zao waweze kununua vitambulisho hivyo kwa faida yao.
Mkuu wa wilaya alisema, baada ya kubaini elimu haijawafikia wajasiriamali wadogo kuchangamkia vitambulisho 5,000 alivyopokea tangu zoezi hilo lianze.Hivyo alisema , kuanzia Januari 26, mwaka huu aliamua kuchukua muda wa mchana kwenda mwenyewe maeneo mbalimbali kutoa elimu kwa wafanyabiashara wadogo na kuuza vitambulisho hivyo kwa wale waliokamilisha ujazaji wa fomu maalumu zilizotolewa.
Chonjo alitaja baadhi ya maeneo hayo ni Stendi ya mabasi Msamvu , eneo la Kingolwira, Mazimbu katika Manispaa ya Morogoro pamoja na halmashauri ya wilaya ya Morogoro eneo la Mkambarani na Mikese .
Alisema kuwa, kasi ilikuwa ni ndogo kwani hadi kufikia Januari 26, mwaka huu ni vitambulisho 581 pekee vilichukuliwa na walengwa kwa gharama ya Sh 20,000 kila kimoja.“ Elimu haijawafikia wajasiriamali wadogo , kwani tangu nimepokea vitambulisho 5,000 hadi Januari 26 mwaka huu vilivyonunuliwa vilikuwa ni 581 idadi hii ilikuwa ni ndogo “ alisema Chonjo.
Hivyo alisema , baada ya kuona mapungufu hayo kuanzia Jumatatu ya Januari 28, Mwaka huu majira ya saa nane mchana aliamua kwenda eneo la kibiashara la Msamvu na hadi kufikia saa 9: 30 alasiri alikuwa tayari ameuza vitambulisho 202.
Mkuu huyo wa wilaya alisema ,vijana wajariliamali zaidi ya 300 walijitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuzijaza ili wapate vitambulisho ambapo zoezi hilo lilifanyika pia katika eneo la kibiashara la Kingolwira kwa kutoa elimu na walengwa zaidi ya 180 walichukua fomu na kujaza.
Pamoja na hayo alisema ,alitaja hatua nyingine aliochukua ni kukutana na watendaji wa kata 29 za Manispaa na kila mmoja kupatiwa vitambulisho 100 na kutakiwa kuviuza hadi Februari 3, mwaka huu .
Hivyo alisema ,ili kufanikicha zoezi hilo Madiwani ni watu muhimu kwa vile ni wawakilishi wa wananchi wao katika Kata wanazotoka , hivyo ni vyema wakajitokeza kuhamasisha vijana , akina mama na watu wengine walengwa wa mpango huo ili wanufaika kutobughudhiwa wanapokuwa kwenye biashara zao.
“ Nawaomba Madiwani mshiriki kutoa elimu kwa wananchi wenu kwa kushirikiana na watendaji ili walengwa wanunue vitambulisho hivyo , kwani fomu ni bure na kitambulisho ni Sh 20,000” alisema Chonjo.
Naye Meya wa Manispaa , Pascal Kihanga baada ya mkuu wa wilaya kutoa ujumbe huo alimhakikishia kuwa , Madiwani watashiriki kikamilifu kuhamasisha na kutoa elimu kwa walengwa ili waweze kuwa na vitambulisho hivyo kwa kuwa suala hilo litawasaidia kuwaondolea usumbufu wakati wa kufanya biashara zao.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa