Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Regina Chonjo amezindua rasmi kampeni ya Furaha yangu leo tarehe 10/11/2018 Manispaa ya morogoro.Kampeni hiyo yenye lengo la kuhamasisha wananchi kupima VVU na iwapo mtu akigundulika kuwa na maambukizi anaanzishiwa dawa mapema.
Akihutubia kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo, Mhe Chonjo amesema kuwa hii inafuatia agizo la Waziri Mkuu Mhe Kasim Majaliwa aliyoizindua mkoani Dodoma mwezi Juni kwa lengo la kuhamasisha wananchi na hasa wanaume kujitokeza na kupima VVU.
Alisema kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha ifikapo 2020 watu wote wawe wamepima VVU,watakaogundulika kuwa na maambukizi ya VVU wawe wameanza kutumia ARV na watakao kuwa wanatumia ARV wawe wamefubaza VVU.
"Kampeni ya Furaha yangu,Pima,Jitambue,Ishi inahamasisha mkakati mpya wa serikali wa upimaji wa VVU na kuanza kutumia ARV mapema.Kupitia Furaha yangu ujumbe wa Serikali ni kuwa kutambua hali yako ya VVU huleta amani,na kuanzishiwa dawa ARV kwa wale wenye maambukizi usaidia kuimarisha afya na kupunguza hatari ya kuambukiza VVU wenza wao",alisema Chonjo.
Kampeni hii inawalenga watanzania wote watambue hali zao za maambukizi ya VVU,hususani wanaume na makundi mengine ambayo ni wasichana walio katika umri wa balehe,wanawake vijana wenye umri wa miaka 15-24,akinamama wajawazito na wanaonyonyesha pamoja na watoto wao.
Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa Halmashauri za mkoa wa Morogoro iliyoathirika na janga la UKIMWI na kwa mujibu wa taarifa za upimaji robo ya Julai-Septemba kiwango ch amaambukizi katika Manispaa kimepungua kutoka asilimia 3.7 na kufikia asimilia 3.5 kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49.
Naye mganga mkuu wa Manispaa Baraka Jonas alisema takwimu zinaonyesha kiwango cha upimaji wa VVU Manispaa bado kipo chini kwa wanaume ikilinganishwa na wanawake,ambapo katika robo mbili zilizopita jumla ya waliopima VVU walikuwa 142,336 kati yao wanaume ni 57,272 saw na asilimia 40.2 na wanawake walikuwa 85,966 sawa na asilimia 59.8.
Hali hii ni hatari kwa afya ya watu hao na familia,kaya na taifa kwa ujumla kwani inadhoofisha mapambano dhidi ya UKIMWI nchini na kulifanya taifa letu letu kutofikia malengo ya kutokomeza ugonjwa,alisema Mganga mkuu Jonas.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya Fikiri Juma akizungumza katika uzinduzi huo amesisitiza kampeni hiyo kutoishia ngazi ya Manispaa bali ishushwe ngazi ya kata,mitaa na badae mitaa ili kutoa hamasa kwa watu wengi zaidi kupima afya zao na kujitambua. Aidha amewatahadharisha wananchi kuachana na tabia hatarishi pamoja na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa