KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ,ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mhe. Mathayo Masele,amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ,Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kurudisha mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Serikali za Mitaa ( SHIMISEMITA) .
Kauli hiyo ameitoa Oktoba 24/2022 katika uzinduzi wa michuano hiyo katika Uwanja wa Mpira wa Miguu wa Jamhuri Morogoro ambapo michuano hiyo imelenga kushirikisha Halmashauri zote hapa nchini.
Akizungumza na Wanamichezo katika uzinduzi huo, Mhe. Masele, amesema michuano hiyo ilisimama takribani miaka 8 hivyo wanamichezo wana kila sababu ya kumpongeza Mhe. Samia kwa maamuzi ya kuiendeleza michezo iyo na kukuza michezo nchini.
Aidha, Mhe. Masele,amewataka wanamichezo wanaoshiriki mashindano hayo kucheza michezo kwa uungwana na upendo na kutumia michezo hiyo kama sehemu ya kudumisha undugu na mshikamano.
" Rais wetu anatupenda sana, amerudisha michezo hii ili tujenge undugu, lakini hapa tunakutana wataalamu mbalimbali ni vyema tukatumia pia nafasi hii kuelezana fursa zilizopo katika Halmashauri zetu na jinsi ya kujengeana uwezo wa kiutendaji kwa kipindi hiki ambacho michuano inaendelea" Amesema Mhe. Masele.
Pia, katika kuona wanamichezo wanacheza kwa kujituma ili kufikia malengo yao, amesisitizia katika mashindano yajayo watumishi walipwe stahiki zao ili kuinua hali ya ushiriki.
Naye Makamu Mwenyekiti wa SHIMISEMITA , Anjelus Ligwembe, amewataka washiriki kuzingatia nidhamu na kucheza kwa upendo katika mashindano hayo.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ambaye ndiye mwenyeji wa Mashindano hayo, Mhe. Albert Msando , ameishukuru SHIMISEMITA kwa kuichagua Morogoro huku akisema uchumi wa Morogoro utaboreshwa kwa kipindi hiki ambacho michuano inaendelea.
" Nawashukuru sana SHIMISEMITA kwa kuchagua Mkoa wetu na Wilaya yetu ya Morogoro kuwa mwenyeji, nipende kuwahakikishia hali ya usalama na utulivu kwa kipidi chote ambacho michezo inaendelea na kumalizika" Amesema DC Msando.
Michezo hiyo ya SHIMISEMITA imeshirikisha jumla ya Halmashauri 44 ambazo ndizo zimeshiriki licha ya kuzitaka Halmshauri zote nchini kushiriki.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa