Maofisa elimu wa kata za Manispaa ya Morogoro wametakiwa kujituma na kuwa waadilifu katika kazi zao za ukaguzi wa shule za msingi na sekondari ili mapungufu yanayobainika yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati kwa ajili ya kuboresha taaluma shuleni na ufaulu wa wanafunzi.
Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo alisema hayo Augost 29, 2018 kwenye viwanja vya jengo la Manipaa ya Morogoro wakati akikabidhi pikipiki 28 kwa Waratibu elimu kata wa Manispaa .
Piki piki hizo zenye gharama zaidi ya cha Sh milioni sita zimetolewa na Serikali kuu chini ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia wahisani wa mtandao wa “ Global Partnership for Education “ (GPE) kwa ajili ya mpango wa kukuza stadi za kusoma , kuandika na kuhesabu (KKK).
“ Mmepewa nyenzo za usafiri kuwawezesha kufika kwenye ukaguzi wa shule za msingi na sekondari kwa wakati , hivyo muwe waadilifu mnapokagua shule , msirubuniwe na taarifa zenu wasilisheni kwa Mkurugenzi ili changamoto zinazobainika zikiwa za wanafunzi kushindwa kujua kusoma , kuandika na kuhesabu zitatuliwe mapema” alisema Chonjo .
“ Kuanzia sasa hatutaki kusikia visingizio, wala kuona mwanafunzi anamaliza shule lakini hajui kusoma , kuandika na kuhesabu “ alisema Chonjo.
Hata hivyo aliwahimiza waratibu hao kuzitunza pikipiki hizo na kushauri baada ya saa za kazi ni vyema zihifadhiwe katika vituo vidogo vya Polisi Kata ili kuepuka kuibiwa kwani baadhi waratibu wanaishi kwenye nyumba za kupanga.
“ Wekeni kwanza usalama wenu ikiwa na kupata mafunzo ya udereva kwenye taasisi za umma kama Veta , kupata leseni , na kutunza chombo za kufanyia kazi ili kikutunze ” alisema Chonjo.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro , John Mgalula kabla ya kumkaribisha mkuu wa wilaya aliwataka waratibu hao kujituma kwa bidii kufanya kazi kwani kwa sasa hakuna visingizio vya kuchelewa usafiri kwani pamoja na kupewa usafiri huo watapatiwa na mafuta ya uendeshaji.
Naye Ofisa elimu Msingi wa Maniapaa hiyo, Abdul Buheti aliishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kutoa usafiri kwa waratibu elimu kata ambao ni moja ya kuzo kuu katika ufuatiliaji wa maendeleo ya shule za msingi na sekondari za serikali pamoja na shule za watu binafsi katika kuona ubora wa taaluma unakuwa wakiwango cha juu.
Nao baadhi ya waratibu wa elimu kata wa Manispaa hiyo akiwemo Thecla Mbiki kutoka kata ya Kilakala alisema ,kukabidhiwa kwa usafiri huo kutapunguza changamoto za kufuatilia shule za msingi na sekondari na kuwawezesha kufanya kazi kwa bidii zaidi .
Hivi karibuni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia , Profesa Joyce Ndalichako alisema , wizara yake pamoja Tamisemi imewezesha Maofisa elimu kata kwa kuwapatia pikipiki zipatazo 2,864 katika wilaya 156 ili waweze kufanya ufuatiliaji wa ufundishaji na ujifunzaji katika shule zilizopo ndani ya maeneo yao.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa