Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo amelishauri Baraza la Madiwani la Manispaa ya Morogoro kutenga fedha za ujenzi wa shule mpya za Sekondari na kulitaka kuhakikisha wanafunzi wote waliochanguliwa kidato cha kwanza mwaka 2019 wanakuwa madarasani katika muda uliopangwa .
Chonjo alisema hayo kwenye kikao cha dharura cha baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo kilichokutana na kufikia maazimio ya kukutana na wadau wa maendeleo ili kuwashirikisha katika kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Lengo ni kwa ajili ya kukabiliana na wimbi kubwa la wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka huu.
“ Pamoja na mipango yetu ya muda mfupi ya sasa ya kukabili changamoto hii , pia ni baraza hili sasa lipange mkakati wa kuwa na bajeti ya kujenga shule mpya za sekondari ili tuondokane na na changamoto za kila mwaka za upungufu wa vyumba vya madarasa” alisema Chonjo.
Naye Ofisa Elimu Sekondari Manispaa ya Morogoro George Obutu ,alitoa taarifa yake kwenye kikao hicho alisema ,madarasa yaliyopo ni 65 na upungufu ni madarasa 60 .
Alisema , licha ya ongezeko la wanafunzi, bado kuna umuhimu wa wazazi na wadau wengine wa maendeleo ya sekta ya elimu kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na umaliziaji wa maboma ya yaliyotelekezwa kwa muda mrefu.
Hata hivyo alisema ,fedha za kumalizia vyumba vya madarasa katika shule saba za sekondari tayari zimepelekwa na hatua ya ujenzi huo unaendelea kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi waliochanguliwa wote kuwa madarasani .
Obutu alisema, hatua za awali zilizochukuliwa ni kuanzisha wanafunzi kusoma kwa awamu mbili kwa siku asubuhi na mchana , lengo ni kuwezesha wanafunzi wote waliochanguliwa kidato cha kwanza wanakuwa madarasani kuanzia Januari 7, mwaka huu.
Nao baadhi ya madiwani walichangia katika kikao hicho kwa nyakati tofauti waliafikiana na maazimio hayo pamoja na kutaka kila mwaka Kata zipatiwe fedha za kuendeleza majengo ya shule za sekondari na shule za msingi kwa kuwa kila mwaka kuna ongezeko kubwa la wanafunzi wanaoandikishwa na kufauli mitihani ya darasa la saba .
Ofisa Elimu mkoa wa Morogoro Mhandisi Joyce Baravuga, kupitia tarifa yake katika kikao cha wadau wa elimu mkoa , alibainisha kuwa , Manispaa ya Morogoro ina mahitaji ya vyumba 129 vilivyopo ni 60 na upungufu ni 69 huku ikiwa imepangiwa jumla ya wanafunzi 6,431 kati yao wavulana ni 3,096 na wasichana 3,335.
Pia Manispaa inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya maabara ambapo mahitaji yake ni 69 na vilivyopo 13 hivyo upungufu ni vyumba 56.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa