Wapima Ardhi wameshauriwa kujiepusha kuwa ni sehemu ya chanzo cha kuzalisha migogoro ya ardhi kwa ajili ya tamaa ya kujipatia fedha kutoka kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo kupitia hotuba ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa Umoja wa wapima ardhi waliosoma Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) uliofanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Chuo hicho mjini Morogoro.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wapima ardhi hao kufanya kazi zao kwa uweledi na uadilifu mkubwa badala ya kuwa wao ni chanzo cha kuendeleza migogoro ya ardhi kutokana na tamaa ya kupata fedha.
“ Kada yenu ina umuhimu kubwa na kwa hiyo muachane na tamaa ya fedha , muwe wa kweli wakati wa kupima ardhi na pale mnapobaini eneo hilo tayari linaonekana limeshapimwa lina milikiwa na mtu mwingine , msichukue fedha , waambieni ukweli wahusika ili kuepusha kuendeleza mgogoro “ alisema Chonjo.
Alisema , kada ya wapima ardhi ina umuhimu wake kwa jamii na inahitajika kuwaletea wananchi maendeleo kwa kuwapimia ardhi na mashamba yao ili kuipa thamani ya ardhi baada ya kupatiwa hati miliki zao.
Mkuu huyo wa wilaya alisema ,wananchi wa Tanzania wanategemea uchumi wao katika kilimo na viwanda , hivyo upimaji wa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na wa mashamba ni muhimu kwa ajili ya kupata hati miliki ili kuongeza thamani ya ardhi .
Alisema kuwa, ardhi yote itakapopimwa itaondoa migogoro kwa vile kila mwenye eneo lake atakuwa ana hati miliki ambayo pia itamsaidia kuitumia kupata mikopo ya fedha kutoka kwenye mabenki kwa ajili ya maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi pamoja na sekta ya viwanda.
Hata hivyo alisema , kutokana na upimaji huo na kuwa na hati miliki, wananchi watakuwa na uwezo wa kuzitumia kwa ajili ya kuombea mikopo katika taasisi za fedha ili waweze kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara sambamba na miradi mingine ya kiuchumi.
Awali , risala ya Umoja wa wapima ardhi waliosoma Chuo cha Ardhi Morogoro, iliyosomwa na Katibu wa Arimo Group , Maliki Mang’indo alisema umoja huo umeiomba Serikali kupitia upya sheria ya usajili wa wapima na kampuni.
Alisema , Arimo inashauri sheria mpya iweze kuweka utaratibu unaruhusu kila mpima ardhi asajiliwe kwa ngazi ya elimu yake na wenye mitaji walioanzisha kampuni waweze kusajili kampuni zao katika bodi ya halmashauri ya wapima ili kuleta ushindani sawa katika soko.
Kwa mujibu wa katibu wa umoja huo kuwa , hadi sasa una wanachama 290 baada ya kuanzishwa mwaka 2013 na kusajiliwa mwaka 2016 kwa madhumuni ya kutatua changamoto za upimaji ardhi, kutoa ushauri juu ya upimaji bora wa ardhi , kubuni, kuratibu na kuaznisha miradi mbalimbali kwa manufaa ya wanachama na wananchi kwa ujumla .
Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro
Anuani: 166 morogoro
Simu: 0232614727
Simu: 0734-039300
Baruapepe : info@morogoromc.go.tz
Hatimiliki ©2017 Halmashauri ya Manisaa ya Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa